Serikali Yatoa Tamko Kuhusu Mauaji ya Watu Saba wa Familia Moja Huko Mwanza

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto imesikitishwa na tukio la mauaji ya watu saba wa familia moja waliokatwakatwa mapanga baada ya kuvamiwa nyumbani, katika kijiji cha Sima wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, siku ya Jumatano usiku.


Wizara inalaani vikali mazingira ya mauaji ya watu hao wa familia moja, ambapo wauaji walivamia nyumba ya mama mjane na kumuuwa yeye mwenyewe, na watu wengine sita wakiwemo watoto watatu.


Wizara inapongeza utayari wa uongozi wa mkoa wa Mwanza na jeshi la Polisi amabo waliweza kufika sehemu ya tukio ili kufuatilia mauaji hayo. Ni imani ya Wizara kuwa Polisi kwa ushirikiano wa wananchi wa wilaya ya Sengerama wataweza kuwasaka watuhumiwa wa mauaji na kuwachukulia hatua kali.


Wizara inawasisitiza wananchi kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuwamata watuhumiwa ili kuondoa hofu miongoni mwa familia za kijiji cha Sima na wilaya ya Sengerema. Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kutarejesha imani na utulivu miongoni mwa wakazi wa Sengerema na hivyo kuweza kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa.


Wizara inasisitiza kwamba kila binadamu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa Sheria za nchi. Vitendo vya mauaji ya kikatili vinapotokea katika familia zetu vinasababisha hofu kubwa miongoni mwa wanafamilia. Mauaji hayo yanawakosesha amani wanafamilia na yanadhohofisha ari ya ndugu wa familia kufanya shughuli zao kwa amani.


Wizara inaomba wanafamilia waliopoteza ndugu zao kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki cha majonzi makubwa, wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kuwasaka watuhumiwa wa mauaji hayo.


Erasto T. Ching’oro (Msemaji)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
12/5/2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post