TAKUKURU Yamkamata Kwa Rushwa Mjumbe FEKI wa Tume Ya Rais Magufuli ya Kuhakiki Watumishi Hewa Shinyanga




Wakati serikali ikiendelea na operesheni ya sukari na watumishi hewa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Shinyanga (TAKUKURU) imemkamata mtu anayejiita Dr. Nyamhanga Malegesi kwa kosa la kuomba rushwa ya shilingi 150,000/= kutoka kwa mwalimu (jina linahifadhiwa) ili aweze kumsaidia kuweka nyaraka zilizokosekana kwenye jalada lake la utumishi “personal file” wakati wa zoezi la uhakiki wa watumishi hewa.


Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Gasto Mkono amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamemkamata mtu huyo jana.

Mkono amesema mtu huyo ambaye kwa jina jingine anaitwa Ezius Maelegesi ili kutimiza uhalifu huo alijifanya ni mjumbe wa tume iliyoundwa na rais John Pombe Magufuli kufanya uhakiki wa watumishi hewa mkoani Shinyanga.

“Mbali na kuomba rushwa ya 150,000/=,pia kutokana na kujifanya mjumbe wa tume,mtu huyo ametenda kosa jingine la kujifanya mtumishi wa umma chini ya kifungu cha 100 (b) cha sheria ya kanuni za adhabu sura 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002”,ameeleza Mkono.

Mkono ameongeza kuwa baada ya mtu huyo kukamatwa na kufanyiwa upekuzi alikutwa na nyaraka mbalimbali zikiwemo CV zilizoambatana na vyeti vya elimu vya watu mbalimbali,CD za hotuba za viongozi wan chi na vitambulisho mbalimbali.

Amesema uchunguzi bado unaendelea kutokana na kuonekana kuwa mtu huyo ni mhalifu mzoefu.

Hata hivyo Mkono amewataka watumishi wote wa umma,wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuwa makini ili wasirubuniwe na wahalifu hasa katika kipindi hiki ambacho kuna operesheni ya sukari na watumishi hewa.

Aidha ametahadharisha kuwa hakuna afisa yeyote wa TAKUKURU au mjumbe au kikosi kazi maalum atakayefanya kazi kwa kificho bila kitambulisho hivyo kwa yeyote atakayetilia shaka watendaji hao atoe taarifa kwa mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga simu namba 0766 388 621 au 0784 511 161,jeshi la polisi au kwa kiongozi yeyote wa serikali mapema iwezekanavyo.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post