Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema tatizo la sukari nchini limetokana na uamuzi usio sahihi wa Rais Dk. John Magufuli, kwa kupiga marufuku uingizwaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi bila kufanya tathmini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri Kivuli wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu, alisema agizo hilo lilitolewa kwa kukurupuka na ndilo lililosababisha sukari kuadimika.
Komu ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini, alisema kama malengo ni kulinda viwanda vya ndani, basi lisifanyike kwa sukari pekee kwa sababu viwanda vipo vingi na bado bidhaa zinaingia kutoka nje nchi.
Alisema kuna harufu ya upendeleo kutokana na Rais kuwa swahiba wa Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye ni mmiliki wa mashamba ya Mtibwa, hivyo amefanya hivyo kwa kupewa ushauri mbaya huku nchi ikiingia kwenye upungufu mkubwa wa sukari.
Alihoji kwa nini apige marufuku kwenye sukari tu wakati kuna viwanda vya nondo, saruji na vinginevyo na vinaleta bidhaa kutoka nje.
Alisema kilichofanywa na Rais ni kukurupuka na ni kuvunja sheria.
Komu alisema kitendo cha Rais kutoa amri ya walioficha sukari wany’ang’anywe, ni kupora haki za watu na kuua mitaji yao kibiashara.
“Hakuna sheria ambayo inaruhusu kwenda kukagua maghala ya wafanyabiashara na kugawa bidhaa bure, hii hali hata wawekezaji wataogopa kuja kuwekeza nchini kwa sababu wataona mazingira ya hapa nchini ni hatarishi," alisema Komu.
Alisema serikali iandae njia mbadala ya kuwafidia watu walionyang’anywa maana wengine wamekopa kwenye taasisi za kifedha.
“Agizo la Rais lina walakini, kwani ni nani katika biashara za watu...tunakokwenda ni kubaya kwani upungufu wa sukari ulijulikana tangu Februari, lakini akapiga marufuku sukari kutoka nje,” alisema Komu.
Alisema katika tafiti mbalimbali ikiwamo ripoti iliyotolewa na Shirika la BBC, mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 590,000, lakini uwezo uliopo ni tani 300,000, hivyo serikali ilikuwa ni busara iruhusu kuingizwa kwa sukari kwa sababu viwanda vya ndani vimekosa uwezo.
Alisema Rais anatakiwa kukemewa na kuambiwa kwamba anakwenda kinyume na kwamba wao kambi ya upinzani hawatetei wanaoficha sukari, lakini serikali itafute namna ya kukabili hali hiyo.
Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema taifa lina viwanda vinne vikubwa vya sukari, lakini bado havina uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha.
Alisema serikali imefanya sukari ionekane kama dawa za kulevya kutokana na kuadimika huko.
Alisema sukari hadi iletwe nchini, ni takriban wiki tano na wanaoingia kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani watahitaji sukari kushinda vitu vingine.
“Sisi hatutetei walioficha, lakini wamenunua ili kuuza kwa taratibu kulingana na bei ya soko wasibughudhiwe maana kuna hatari ya benki kushindwa kurejeshewa fedha zilizokopwa,” alisema Kubenea.
Social Plugin