Wakazi wa Kata ya Karansi, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro wametoa uamuzi kuwa wanawake watakaovaa sketi fupi na vijana watakaovalia suruali chini ya kiuno, wataadhibiwa kwa kuchapwa viboko 60 hadi 70.
Uamuzi huo umefikiwa na wakazi zaidi ya 200 wakisema uvaaji huo ni kinyume na mila na desturi za Kiafrika.
Vazi lingine lisilotakiwa kwa wanawake ni kuvaa suruali pamoja na vijana kunyoa ndevu mitindo isiyofaa.
Mkutano huo ulioandaliwa na wazee wa kimila jamii ya Meru (Wachili) na Wamasai (Malaigwani), uliwavutia wananchi wengi ambao walihudhuria.
Sambamba na uamuzi huo utakaokuwa unafanyika hadharani, pia adhabu hiyo itawahusu wezi wa mali na wanaopenda kucheza pool table wakati wa kazi.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Wilbrod Mutafungwa alipinga uamuzi huo akisema kwa maazimio hayo ya kuwaadhibu watuhumiwa kwa kuwachapa viboko ni kujichukulia sheria mkononi na ni kinyume na sheria.
Social Plugin