Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Wachungaji Wawili Wa Kanisa La KKKT Wafikishwa Mahakamani Kwa Tuhuma za Mauaji Huko Moshi


Wakati mchungaji wa Kanisa la Moravian akikamatwa na meno ya tembo 11 ndani ya kanisa, huko Moshi wachungaji wawili wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji. 




Tukio la wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro linawahusisha wachungaji wawili wa KKKT, Rodrick Mlay (52) na Godbess Mamkwe (38) pamoja na wananchi watatu ambao jana walipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini humo kwa madai ya kuua kwa kukusudia. 




Wakati wachungaji hao wawili wakipanda kizimbani, Polisi mkoani Katavi kwa kushirikiana na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi wanawashikilia watu wawili akiwamo mchungaji wa Kanisa la Moravian kwa tuhuma ya kunaswa wakiwa na meno ya tembo 11 wakiwa wameyahifadhi ndani ya kanisa. 




Akizungumzia meno hayo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi katika Kanisa la Moravian lililopo Kijiji cha Usevya, Wilaya ya Mlele. 




Nyanda alisema mchungaji huyo akiwa na mwenzake ambao wote majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za upelelezi, walikamatwa kufuatia taarifa zilizolifikia jeshi hilo na askari wa hifadhi kuwa, watu hao wanajihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo na wamekuwa wakiyahifadhi ndani ya kanisa. 




Baada ya taarifa hizo, polisi na askari hao walifanya uchunguzi kuhusiana na taarifa hizo kwa kufika katika kanisa hilo na kufanya upekuzi uliofanikisha kukamatwa kwa meno hayo yakiwa yamehifadhiwa kwenye tenga la kubebea mizigo. 




Kaimu kamanda huyo alisema katika matukio mengine mawili tofauti yaliyotokea Mei 8, saa mbili usiku kwenye maeneo ya Mgolokani, Kata ya Sitarike wilayani humo, polisi kwa kushirikiana na askari wa hifadhi hiyo walimkamata mtu mmoja akiwa na jino moja la tembo. 




Nyanda alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya askari kufanya upekuzi ndani ya nyumba yake na kukamata jino hilo na lingine la simba. 




Alisema wote waliokamatwa kwenye matukio hayo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote ili kujibu tuhuma zinazowakabili. 




Katika tukio la wachungaji waliofikishwa mahakamani mjini Moshi, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Julieth Mawole alisema wakiwa na wananchi watatu aliowataja kwa majina ya Fadhili Mkenda (36), Jackson Ruben (45) na Mathayo Moses (27), Mei 4 katika eneo la Kilema Pofo wanadaiwa kumuua kwa makusudi Frank Peter (19). 




Hakimu Mawole aliwataka watuhumiwa hao kutojibu lolote na kesi dhidi yao itasikilizwa Mei 23 katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na wote walipelekwa rumande kwa sababu shtaka waliloshtakiwa nalo halina dhamana kisheria.




Katika hatua nyingine, raia wa Marekani, Mbaraka Mtambo (50) amekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na maganda mawili ya kobe bahari aliyokuwa ameyafichwa kwenye begi la nguo. 




Kamanda wa Polisi wa JNIA, Martin Otieno alisema raia huyo mwenye asili ya Tanzania, alikamatwa juzi saa 3.45 usiku akijiandaa kwa ajili ya safari ya kwenda Marekani na ndege ya Shirika la KLM kupitia Uholanzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com