Wahitimu Sita wa Mafunzo ya JKT Wafikishwa Mahakamani Sakata la Kudai Ajira



WAHITIMU sita wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kufanya mkusanyiko usio halali na kushawishi wenzao kuandamana kwenda Ikulu kudai ajira, anaandika Faki Sosi.


Washtakiwa katika kesi hiyo ni George Mgoba, mwenyekiti wao; Parali Kiwango, makamu mwenyekiti; Linus Steven, katibu wa umoja wa wahitimu hao na wahitimu wengine, Emmanuel Mwasyembe, Ridhiwani Ngowi na Jacob Mang’wita.


Akiwasomea mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Benard Kongola amesema, washitakiwa hao wanadaiwa kwamba 15 Februari 2014 katika eneo la Msimbazi Centre, Ilala Dar es Salaam walipanga njama za kutenda makosa hayo.


Katika shitaka lingine watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kuandamana kwenda kwa Rais kulazimisha kupewa ajira katika utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kwamba, hatua hiyo ingesababisha uvunjifu wa amani.


Kwa upande wa mshitakiwa Mgoba, Kiwango na Steven, wanadaiwa siku hiyo katika eneo hilo, walishawishi wahitimu wenzao wa mafunzo ya JKT, kufanya maandamano kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika utumishi wa umma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.


Washtakiwa hao wamepandishwa kizimbani ikiwa ni siku chache baada ya kesi dhidi yao kufutwa na kuachiwa Mei 26, mwaka huu kisha kukamatwa tena na leo kupandishwa mahakamani kwa mashtaka hayohayo.


Katika kesi ya awali iliyokuwa ikisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, tayari mashahidi saba walikuwa wameshatoa ushahidi mahakamani hapo huku akiwa amebakia shahidi mmoja tu ili kufunga ushahidi ndipo kesi hiyo ilipofutwa na watuhumiwa hao kukamatwa tena na kusomewa mashtaka hayo.


Watuhumiwa hao wamerudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Juni 9 Mwaka huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post