Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Wahukumiwa Kifungo Jela Miaka 12 Kwa Kujifanya Maafisa wa Jeshi la Polisi na Kutapeli Huko Katavi



MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi imewahukumu Alex Chotala(24) na Gabriel Katabi (25) wote wakazi wa mji wa Mpanda kifungo cha miaka 12 jela baada ya kupatikana na kosa la kujifanya maafisa wa jeshi la Polisi na kutapeli fedha kiasi cha shilingi 800,000.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 27 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Odira Amworo baada ya Mahakama hiyo kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo .

Awali katika kesi hiyo Mwanasheria wa Serikali Mkoa wa Katavi Malifimbo Hongera alidai mahakamani kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Agosti 31 mwaka jana katika Kijiji cha Kapanga Tarafa ya Mwese Wilayani humo.

Alidai kuwa washitakiwa walijitambulisha kwa msichana aitwaye Vishiti Mkono(21) mkazi wa Kijiji cha Kapanga kuwa wao ni maafisa wa jeshi la Polisi Wilaya ya Mpanda na kutokana na vyeo walivyo navyo wanauwezo wa kumsaidia kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa JKT hivyo walimtaka afike katika kituo cha polisi cha Mpanda Mjini akiwa na cheti cha kuzaliwa na vya kumalizia shule na walimpatia namba za simu ili akifika awapigie.

Malifimbo aliieleza Mahakama Vishiti alifanya kama ambavyo alivyoelekezwa na washitakiwa na siku waliyokubaliana alipofika aliwapigia simu washitakiwa ambao walimtaka wamkute nyuma ya jengo la kituo cha polisi cha Mpanda mjini kwa kile walichodai ofisini kwao kulikuwa na kikao kinaendelea cha maafisa wa polisi.

Washitakiwa hao walifika nyuma ya jengo hilo na kumtaka awapatie vyeti walivyokuwa wamemuagiza na baada ya kuwapatia walimweleza Dada huyo awapatie kiasi cha Tsh 800,000 kwa kuwa cheti chake chake ni cha darasa la saba ili fedha hizo wakawapatie maafisa wenzao wa jeshi la Wananchi ambao wanahusika na usaili.

Vishiti alifanya hivyo na ndipo walipomchukua na kwenda nae eneo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mpanda kwa lengo la kupeleka vyeti na walimuacha hapo barabarani kwa zaidi ya saa nne kisha walirudi na kumwambia kuwa vyeti vyake vimepokelewa na kukubaliwa.

Baada ya kupeleka vyeti hivyo na fedha mtuhumiwa Katabi alifuatana na msichana huyo mpaka katika nyumba ya kulala wageni ambapo walilala wote na kisha kushirikiana kimapenzi kwa madai kuwa atafanya kila liwezekanalo hadi apate nafasi ya kujiunga na jeshi hilo.

Mwanasheria huyo alieleza siku iliyofuata Dada huyo alirudi Kijijini kwao Kapanga ambako alikuwa akifanya kazi ya kuuza duka la dawa za Binadamu wakati akiwa anasubiri muda ufike wa kwenda kujiunga na jeshi la kujenga Taifa .

Baada ya wiki moja washitakiwa walimtumia barua ambayo ilikuwa ni yakughushi ikiwa inaeleza kuwa amechaguliwa kujiunga na jeshi la kujenga Taifa Itende Mbeya barua ambayo ilitolewa mahakamani hapo kama kielelezo .

Hakimu Mkazi Odira Amworo kabla ya kusoma aliiambia Mahakama kuwa washitakiwa wote wawili wamepatikana na hatia ya makosa manne kati ya matano waliokuwa wameshitaki hivyo kama wanayosababu ya msingi ya kuweza kuishawishi Mahakama iwapunguzie adhabu wanapewa nafasi ya kujitetea.

Washitakiwa katika utetezi wao waliiomba Mahakama iwapunguzie adhabu kwa kuwa umri wao bado ni mdogo na wanatarajia kuoa hivi karibuni .

Akisoma hukumu hiyo Hakimu alieleza Amworo katika kosa la kwanza la kujifanya maafisa wajeshi la Polisi Mahakama imewahukumu kifungo cha miaka mitatu jela ,Kosa la Pili la kufoji barua kifungo cha miaka mitatu,kosa tatu kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kifungo cha miaka mitatu na kosa la nne kujifanya matapeli kifungo cha miaka mitatu.na kosa la tano la kufanya mapenzi kwa njia ya ulaghai waliweza kuondolewa kwa kukosekana ushahidi wa kutosha

Hakimu huyo alisema makosa hayo yote adhabu yake inakwenda pamoja hivyo washitakiwa watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela kuanzia juzi na kulipa fedha Tsh 800,000 walizotapeli ili arudishiwe aliyetapeliwa.
 Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com