Walimu Wanawake Mkoani Katavi Wacharuka ,Waiomba Serikali Kuheshimu Sheria Ya Ndoa


Walimu Wanawake Wilayani Mpanda Mkoa wa Katavi wameiomba serikali kuheshimu sheria ya ndoa ambayo inaruhusu mtumishi anapofunga ndoa kumfuata mwenzi wake ili waishi pamoja kutokana na waajiri kuipuuza na kuwanyima uhamisho hivyo kumechangia ndoa nyingi kuvunjika .


Maombi hayo ya walimu wa wanawake kwa serikali yalitolewa juzi na walimu viongozi wanawake sehemu ya kazi wakati wa mafunzo ya siku moja yaliofanyika katika ukumbi wa chekechea wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda na kufunguliwa na mwenyekiti wa Chama Cha Walimu (CWT) wilaya ya Mpanda Jumanne Msomba.


Mafunzo hayo ya siku moja yaliondaliwa na CWT Wilaya ya Mpanda yalikuwa na lengo la kuwaelimisha walimu viongozi wa wanawake sehemu ya kazi ili waweze kutmbua haki zao na kuzilinda pamoja na kupatiwa mafunzo ya ujasiliamali ili wajikomboe kiuchumi .

Baadhi ya walimu hao wanawake walieleza kuwa kumekuwepo na tabia kwa waajiri kuwakatalia kuwapa uhamisho walimu wa wanawake pindi wanapokuwa wamafunga ndoa wanapoomba uhamisho wa kuwafuata wenzi wao .

Mmoja wa Walimu hao Siwezi Machulo alieleza kuwa ndoa nyingi za walimu wanawake zimevunjika kutokana na walimu wanawake kunyimwa uhamisho wa kuwafuata wenzi wao hasa wanao kuwa nje ya mkoa wa Katavi .

Alifafanua kuwa mwajiri amekuwa akiwanyima uhamisho wa kuwafuata wenzi wao kwa kile ambacho amekuwa akidai kuwa mwalimu anayetaka kuhamishwa kumfuata mwenzi wake hawezi kuhamishwa hadi hapo atakapokuwa amepata mwalimu mwingine wa kubadilishana naye huko anakotaka kuhamia wakati siyo utaratibu wa Sheria ya ndoa .

Walimu hao wa kitengo cha wanawake sehemu ya kazi wamelalamikia pia tabia ya mwajiri wao ya kuwatengenezea majeneza yaliochini ya kiwango walimu ambao wanao kuwa wamefariki duniani tofauti na watumishi wa idara nyingine wanapokuwa wamefariki majeneza yao yanakuwa na kiwango chenye ubora .

Awali akifungua mafunzo hayo Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Mpanda Jumanne Msomba aliwataka walimu kufanya kazi kwa kufuata taratibu za kazi katika utumishi wao . 


Alisema walimu viongozi wa wanawake sehemu ya kazi wanao wajibu wa kuwaelimisha walimu wafahamu haki zao za msingi kama vile uhamisho wa kuwafuata wenzi wao ,likizo kupandishwa madaraja na kurekebishiwa mishahara. 


Naye Kaimu Katibu wa CWT Wilaya ya Mpanda Masanja Manyanga alisema kuwa hakuna sheria yoyote wala utaratibu unae mzuia mtu aliyefunga ndoa kumfuata mwenzi wake kwa kisingizio cha mpaka awe na mtu wa kubadilishana naye .

Alisema huo ni unyanyasaji wa kijinsia hivyo walimu wenye malalamiko hayo wayafikishe CWT ili waweze kuona namna ya kuyashughulikia kwa mwajiri anayefanya hivyo . 


Kuhusu majeneza ya walimu yanayotengenezwa chini ya kiwango alisema ni jukumu la mwajiri kugharamia gharama za mtumishi hivyo sio suala la hiari bali ni haki ya mtumishi hivyo pindi wanapoona mwalimu mwenzao ametengenezewa jeneza lililo chini ya kiwango walikatae kulipokea .

Na Walter Mguluchuma -Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post