JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu 14 wakiwamo wanawake wawili na mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Mwika wilayani Moshi, kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha.
Miongoni mwa watuhumiwa hao wapo wanaodaiwa kuwa majambazi sugu 10, waganga wa kienyeji wawili ambao walikuwa wakitumika kwa ajili ya kuwapa dawa watuhumiwa hao ili wasikamatwe na polisi na kuzindika silaha zilizokuwa zikitumika katika ujambazi na wanawake wapishi wa watuhumiwa hao wakiwa mafichoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mtafungwa alisema jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Tanga na Kilimanjaro kufuatia msako mkali wa askari uliotokana na taarifa za siri.
Mtafungwa alisema mwanafunzi wa sekondari ya Mwika, Kelvin Shayo (17) miongoni mwa matukio anayotuhumiwa kushiriki ni pamoja na la kumpora bastola yenye namba YP0466 Tz Car aina ya brown, askari mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Elibariki Urio (67).
Kamanda alisema silaha hiyo iliporwa Februari 25 mwaka huu baada ya majambazi kumvamia nyumbani kwake na kupora mali pamoja na silaha hiyo kisha kwenda kuificha nyumbani kwa Eleutery Nguma (62) mkazi wa Makami Chini, Tarafa ya Vunjo ikiwa imefukiwa ardhini kwenye mfuko wa plastiki.
Aidha, Mtafungwa alisema kwa mujibu wa kumbukumbu za polisi mtuhumiwa huyo (Nguma) ilidhaniwa kuwa ameacha vitendo vya ujambazi lakini amebainika kuwa ni mpangaji wa njama za ujambazi, kuficha mali za wizi pamoja na kuficha silaha zinazotumika katika uhalifu.
Social Plugin