Watu wawili wakazi wa vijiji vya Tunungo na Dutumi tarafa ya ngerengere wamenusurika kifo mara baada ya kuvamiwa na mamba kwa nyakati tofauti wakati wakijaribu kuvuka Mto Ruvu unaopita katika baadhi ya vijiji vilivyopo katika wilaya ya Morogoro.
ITV imefika katika chumba cha majeruhi kilichopo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro na kuzungumza na majeruhi hao ambao wamesema walikumbwa na kadhia hiyo kwa nyakati tofauti katika mto huo ambao unadaiwa kuwa na kiasi kikubwa cha mamba ambapo baada ya kuvamiwa walipiga kelele ambazo zilisaidia kupatikana kwa wasamalia wema waliofika na kufanikiwa kuwaokoa.
Kwa upande wake muuguzi wa zamu Renfrida Mwarabu amesema walimpokea mgonjwa huyo akiwa katika hali mbaya na kwamba anaendelea kupatiwa matibabu huku baadhi ya wananchi wanaoishi katika kijiji hicho wakiiomba serikali kutatua kero ya daraja ambalo limekuwa halipitiki na kusababisha watu kuvuka kwa kuogelea huku wakihatarisha maisha yao kutokana na mto huo kuwa na mamba wengi.
Via>>ITV