WIZARA ya Nishati na Madini imetengewa Sh trilioni 1.22 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 huku fedha za miradi ya maendeleo zikiwa ni asilimia 94 ya fedha hizo.
Pia katika kuongeza kiwango kikubwa cha uzalishaji wa nishati, kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa, asilimia 98 ya Bajeti ya Maendeleo imetengwa kwa ajili ya sekta ya nishati.
Aidha, serikali imeongeza bajeti ya maendeleo ya fedha za ndani kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kufikia Sh bilioni 534.4, huku wateja wa umeme wa REA na Tanesco wakifikia 220,128. Mbali na hayo, kiwango cha upatikanaji wa huduma ya umeme kimeongezeka kufikia asilimia 40.
Hayo yalisemwa bungeni jana mjini Dodoma na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2016/17.
Profesa Muhongo alisema bajeti ya wizara kwa mwaka 2016/17 ni Sh trilioni 1,22,583,517,000, na kati ya fedha hizo, Sh 1,056,354,669,000 ni fedha za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 94.
“Kwa kuzingatia Ibara ya 43(a) ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 inayoelekeza serikali kuongeza kiwango kikubwa cha uzalishaji wa nishati ili kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa, asilimia 98 ya Bajeti ya Maendeleo imetengwa kwa ajili ya sekta ya nishati,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema katika mwaka wa fedha 2015/16, waliidhinishiwa na Bunge Sh bilioni 642.12, na kati ya fedha hizo, Sh bilioni 502.30 sawa na asilimia 78 ya bajeti yote zilikuwa ni bajeti ya maendeleo.
“Hata hivyo, Bajeti hiyo iliongezeka kutoka shilingi bilioni 642.12 hadi shilingi bilioni 762.12. lengo la ongezeko ni kutekeleza miradi mikubwa ya kufua umeme ukiwemo Mradi wa Kinyerezi II – MW 240 ili kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini,” alisema Profesa Muhongo.
Megawati zaongezeka
Akizungumzia sekta ndogo ya umeme, alisema uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umeongezeka kutoka megawati 1,226.24 Aprili, 2015 hadi kufikia megawati 1,461.69 Aprili, 2016 sawa na ongezeko la asilimia 19.
“Ongezeko hilo limechangiwa na mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia baada ya kukamilika kwa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam,” alisema.
Aidha, alisema mahitaji ya juu ya umeme yameongezeka kutoka megawati 988.27 Desemba, 2015 hadi kufikia megawati 1,026.02 Machi, 2016 sawa na ongezeko la asilimia nne.
Kuhusu upatikanaji wa umeme nchini, alisema kiwango cha huduma ya upatikanaji wa umeme kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka.
“Watanzania waliofikiwa na huduma hiyo wameongezeka kutoka asilimia 36 mwezi Machi, 2015 hadi kufikia takribani asilimia 40 mwezi Aprili, 2016.
“Ongezeko hilo limetokana na juhudi za serikali za kusambaza umeme nchini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),” alisema Profesa Muhongo.
Alisema kuanzia Julai, 2015 hadi Aprili, 2016 idadi ya wateja waliounganishwa na umeme wa REA pamoja na Tanesco ni 220,128 sawa na asilimia 88 ya lengo la kuunganisha wateja 250,000 ifikapo Juni mwaka huu.
Umeme bila MCC
“Katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa umeme vijijini, serikali imeongeza Bajeti ya Maendeleo ya fedha za ndani kwa REA kutoka shilingi bilioni 357.12 kwa mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 534.4 kwa mwaka 2016/17. Tumeongeza asilimia 50 na hakuna fedha za MCC (Shirika la Changamoto za Milenia) hapa,” alisema Muhongo.
"Ongezeko hilo ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020. Aidha, fedha za nje zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo ni shilingi bilioni 53.21 sawa na asilimia tisa na hivyo kufanya jumla ya bajeti yote ya REA kwa mwaka 2016/17 kuwa shilingi bilioni 537.61.”
Mitambo kuongezwa
Akizungumzia miradi ya kuzalisha na kusafirisha umeme, alisema serikali itatekeleza miradi mingi ambayo baadhi itakamilika katika mwaka wa fedha 2019/2020.
Alisema katika juhudi za kuongeza uzalishaji umeme, serikali imepanga kuongeza mitambo mingine ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi – I Extension wa megawati 185.
Alitaja mingine ni Kinyerezi II megawati 240, huku akitaja miradi iliyo katika hatua za mwisho za maandalizi ya miradi ambayo ni Kinyerezi III (megawati –MW 300), Rusumo Falls MW 80), Malagarasi MW 45 na Kanoko MW 87.
Kuhusu miradi ya usafirishaji umeme, alisema ujenzi wa mradi wa Iringa hadi Shinyanga wa kilovolti 400 umefikia wastani wa asilimia 89, ambao gharama zake ni Sh bilioni 387.5 na utakamilika Septemba mwaka huu.
Alisema serikali inaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa njia za kusafirisha umeme zenye uwezo mkubwa hususan kilovolti 400.
Miradi ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2019/20 aliitaja kuwa ni Singida – Arusha – Namanga kv 400, Bulyahulu – Geita kv 220, Geita – Nyakanazi kv 220, North East Grid kv 400 na Somanga – Kinyerezi kv 400.
Aidha, alisema mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Somanga Fungu hadi Kinyerezi, Tanesco imeshakamilisha ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi huu.
“Hadi kufikia mwezi Aprili, 2016 shilingi bilioni 26.06 tayari zimelipwa na Tanesco kwa watu 947 katika wilaya za Ilala na Temeke,” alieleza.
Katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini, mwaka 2014 Tanesco ilianzisha Kampuni Tanzu ya Tanzania Concrete Poles Manufacturing Company Limited (TCPCO), kwa ajili ya kujenga viwanda vya kutengeneza nguzo za zege nchini.
“Baada ya kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa viwanda hivyo, TCPCO inatarajia kuanza uzalishaji wa nguzo za zege mwaka 2016/17,” alisema.
Kuhusu punguzo la viwango vya bei za umeme, Profesa Muhongo aliliarifu Bunge kuhusu punguzo hilo lililoanza Aprili mosi, mwaka huu.
Alisema serikali imepunguza bei ya umeme kwa kati ya asilimia 1.5 na 2.4, na pia imeondoa tozo ya kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme ya Sh 5,000 na tozo ya huduma ya mwezi ya Sh 5,520 kwa wateja wa umeme wa Daraja la TI na DI, ambao wengi wao ni wa majumbani.
“Hatua hii itawasaidia watumiaji wadogo wa umeme mijini na vijijini kumudu gharama hizo, hivyo kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi,” alisema Profesa Muhongo aliyerejea katika wizara hiyo baada ya kuwahi kuiongoza katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Kuhusu gesi asilia, alisema kukamilika kwa ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara kupitia Lindi hadi Dar es Salaam kumeongeza mchango wa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia kufikia asilimia 49.
Aidha, alisema uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia umewezesha gharama za uzalishaji umeme nchini kupungua kutoka wastani wa Sh 262 hadi 229 kwa uniti moja ya umeme.
Profesa Muhongo alisema bomba hilo lenye urefu wa kilometa 542 ni pamoja na mitambo ya kusafisha gesi asilia katika maeneo ya Madimba (Mtwara) na Songo Songo (Lindi). Mradi huo ulizinduliwa rasmi Oktoba, 2015 na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Akizungumzia shughuli za utafutaji gesi asilia, alisema Kampuni ya Dodsal imekamilisha tathmini ya kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa katika kisima cha Mambakofi – I kwenye Kitalu cha Ruvu Mkoa wa Pwani. Alisema tathmini hiyo inaonesha uwepo wa gesi asilia kiasi cha futi za ujazo trilioni (TFC) 2.17.
“Hivyo kufanya gesi asilia iliyogunduliwa nchini hadi Mei, 2016 kufikia TCF 57.25 ikilinganishwa na TCF 55.08 zilizokuwepo mwezi Aprili, 2015. Kati ya kiasi hicho, TCF 47.13 zipo kwenye kina kirefu baharini na TCF 10.12 zipo nchi kavu,” alisema.
Akizungumzia usambazaji wa gesi asilia jijini Dar es Salaam, alisema lengo la mradi huo ni kujenga mtandao wa kusambaza gesi asilia kwa njia ya mabomba na iliyoshindiliwa (CNG).