Akiongea kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Afande Sele amesema zamani walikuwa wanatumia rushwa na kujuana ili kuweza kupata air time, lakini sasa wasanii wanatumia skendo ili kujitangaza katika kazi zao.
"Watu wamekosa ubunifu kwenye kazi zao, ile atahari ambayo tulikuwa tunaiona siku za nyuma sasa hivi ndio inajidhihirisha zaidi, watu walikuwa wanapata air time kwa ajili ya rushwa, kujuana, lakini walikuwa hawana ubunifu, kwa hiyo sasa hivi wameamua kutumia kiki za mambo ya mapenzi mapenzi, kwa vile tayari uwezo wao wa kubuni na kusababisha watu wawakubali moja kwa moja kupitia kazi zao unakuwa hakuna" alisema Afande Sele.
Afande Sele amesema kitendo hicho sio kizuri kisipodhibitiwa, kwani kinachangia kwa kiasi kikubwa kuua muziki wa bongo fleva, kwani watu wameshindwa kabisa kuandika mashairi mazuri yenye ujumbe.
"Mtu anakuwa hana uwezo wa kuonyesha uwezo wa kipaji chake moja kwa moja ili kazi zake zisikike lazima atafute namna nyingine ya kusikika na kuonekana, na ndio hiyo kamchukua fulani, mara kazaa na fulani, mara anataka kumuoa fulani, watu wameshindwa kutunga, wameshindwa kushawishi watu", alisema Afande Sele.
Social Plugin