Familia ya marehemu Daniel Lumondo, mkazi wa kijiji cha Kalundye wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, imelishutumu jeshi la polisi mkoani Mwanza kwa madai ya kusababisha kifo cha ndugu yao, baada ya askari polisi wa kituo cha Kirumba wilayani Ilemela kumtia nguvuni kwa tuhuma za kujipatia fedha kiasi cha shilingi milioni moja kwa njia za udanganyifu.
Marehemu Lumondo ambaye wakati wa uhai wake alikuwa akijishughulisha na tiba asili katika eneo la Kirumba jijini Mwanza, alifariki dunia Juni 14 mwaka huu majira ya saa tisa usiku katika hospitali ya rufaa Bugando alikokuwa amelazwa kwa muda wa siku nne kwenye chumba cha wagonjwa mahtuti, chini ya ulinzi mkali wa polisi ambao walimkamata Juni 4 mwaka huu kwa tuhuma za madai ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu toka kwa Ferdinand Mtazi mkazi wa Jijini Mwanza.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ahmed Msangi amethibitisha tukio hilo na kuongeza kwamba jeshi hilo linamshikilia askari wake mmoja kwa mahojiano na uchunguzi zaidi wa kifo hicho.
Hili ni tukio la pili kwa askari polisi kuhusishwa na vifo vya watuhumiwa wa makosa mbalimbali, ambapo mwezi Aprili mwaka huu askari polisi watatu wa kituo cha polisi Muleba mkoani Kagera walidaiwa kumpiga na kumsababisha kifo mvuvi mmoja wa kisiwa cha Kunene wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza Hamis Tabibu Kilangi na mpaka sasa hakuna hatua zozote za kinidhamu na kisheria zilizowahi kuchukuliwa na Jeshi hilo dhidi ya askari hao.
Via>>ITV
Social Plugin