Askofu Gwajima Hajulikani Alipo, Polisi Waendelea Kumsaka Usiku na Mchana
Saturday, June 18, 2016
Baada
ya kuweka kambi kwa zaidi ya saa saba nyumbani kwa Askofu Josephat
Gwajima wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Jeshi la Polisi limesema bado
linamsaka kiongozi huyo wa kiroho usiku na mchana.
Juzi
askari wa jeshi hilo, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam walishinda mbele ya
geti la nyumba ya askofu huyo kwa zaidi ya muda huo bila kufunguliwa na
kuondoka bila kumkamata, hiyo ikiwa ni mara ya pili kwa chombo hicho
cha dola kufanya hivyo katika kipindi cha miezi 16.
Baada ya kushindwa kumtia nguvuni mapema mwaka jana, Askofu Gwajima alijisalimisha kituoni siku iliyofuata.
Lakini jana, Gwajima hakufanya hivyo, na haijulikani alipo. Kamanda wa
Kanda ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema wanaendelea kumtafuta
askofu huyo na kuwataka wenye taarifa za mahali aliko, waisaidie polisi.
Akieleza sababu za kwenda nyumbani kwake bila ya kumtaarifu askofu huyo, Kamanda Sirro alisema hawalazimiki.
“Si lazima apelekewe taarifa, askari walikwenda kwa nia njema ya
kuonana naye ndiyo maana hawakutoa taarifa,” alisema Sirro na kuongeza:
“Kama amejificha, tukimbaini alipo tutamkamata na atambue bado
tunamtafuta.”
Askofu Gwajima anatafutwa na polisi katika
kipindi ambacho mkanda unaodhaniwa una sauti yake, umezagaa kwenye
mitandao ya jamii.
Sauti kwenye mkanda huo inasema Rais
wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete afikishwe mahakamani kwa
yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo rais wa sasa, John
Magufuli anayashughulikia.
Pia, sauti hiyo inadai kuwa
baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka
Magufuli asipewe uongozi wa chama hicho kwa sasa kama ilivyo utaratibu
wa chama hicho.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa
majina yao kwa kile walichodai si wasemaji wa familia wala kanisa, watu
wa karibu na askofu huyo walisema wanashangaa kuona polisi wanamtafuta
bila kufuata taratibu kama kumuandikia barua.
Mmoja wa
watu hao alisema hadi sasa wanashindwa kufahamu kama waliokuja kwa
askofu ni askari kama inavyoelezwa au majambazi kwa sababu hawakuwa na
sare wala vitambulisho.
Alisema sababu anayotafutiwa
Gwajima ni kukinanga chama, wanaomtafuta ni wana usalama ambao
hawatakiwi kuwa na chama kitu ambacho kinatia shaka.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin