Watu watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti, akiwamo aliyeuawa kwa kipigo na kuchomwa moto kwa tuhuma ya kupora simu ya mkononi aina ya Tecno.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema Juni 2, mtu huyo ambaye jina lake halikupatika anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 hadi 30, aliuawa baada ya kumpora simu mpitanjia eneo la Ngaza, Kata ya Nyegezi jijini Mwanza.
“Kabla ya kupora simu mtu aliyejulikana kwa jina la Aanicia Rwezaura alitishwa na yule aliyeuawa kwa panga, lakini wananchi wenye hasira kali walimwandama, kumpiga na hatimaye kumchoma moto hadi kufa,” alisema Kamanda Msangi
Katika tukio jingine, kamanda huyo amesema watu wawili wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea Kijiji cha Isunganh’olo wilayani Sengerema.
Aliwataja waliofariki kuwa ni dereva wa gari aina ya Toyota Prado, Samson Kasala na mwendesha baiskeli, John Manyilizu aliyekuwa akipita pembezoni mwa barabara.
“Gari hilo lililokuwa kwenye mwendo kasi lilipasuka gurudumu na kuacha njia kabla ya kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi,” alisema Msangi
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Mandago Misana, Thobias Kitenge, Jesca Andrew na Mehob Peter ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kwa matibabu.
Kamanda Msangi aliwataka madereva kuwa watulivu barabarani na kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwaonya wale wasiozizingatia kwamba watabanwa kisheria.
Alisema mwendokasi umekuwa chanzo cha ajali nyingi za barabarani ambazo iwapo wahusika wangekuwa makini zingeweza kuepukika.
Social Plugin