Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa
WAKATI jana dunia imeazimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, wimbi la mauaji ya kutisha limeendelea kuliandama Taifa, baada ya baba mmoja kuteketeza familia yake kwa kuwachinja.
Tukio hilo limetokea juzi katika Kijiji cha Mongoroma Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, ambapo baba huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na tuhuma za mauaji hayo.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kwamba, baada ya mauaji hayo, mtuhumiwa huyo alichukua mwili wa mtoto mmoja na kuubanika kwenye moto mkubwa, kisha akaanza kula nyama yake.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alithibitisha tukio hilo lililotokea Juni 14, mwaka huu saa 2 asubuhi katika Kitongoji cha Sakule wilayani humo.
Kamanda Mambosasa alisema mtuhumiwa huyo aliyejulikana kwa jina la Idd Mkirangi mwenye umri wa miaka 30-35, alianza kwa kumuua rafiki yake wa kike (hawara), Tabu Twaha (35) mkazi wa Mtaa wa Ubondeni.
“Alianza kumuua huyu mama ambaye ni rafiki yake kwa kumchinja, kisha akageukia watoto ambao hawana hatia yoyote. Kibaya zaidi baada ya hapo alichukuwa mwili wa mmoja wa wale watoto akautupa kwenye moto mkubwa aliokuwa ameuandaa.
“Kwa lugha nyepesi nisema alianza kumchoma kama mtu anavyochama nyama, baada ya kuona ameiva akaaza kukata mkono na kula nyama,”alisema.
Alisema baada ya hapo, baba huyo aliwakaribisha baadhi ya wananchi waliokuwa jirani ili wajumuike naye kula nyama, ndipo waliposhutukia na kuanza kumshambulia kwa kipigo.
Kamanda Mambosasa aliwataja watoto waliouawa kuwa ni Chamilion Festo (mwaka mmoja) na Amir Seja ambaye umri wake haukufahamika mara moja.
Alisema chanzo cha mauaji hayo ni kwamba, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuvuta bangi nyingi.
“Chanzo cha mauaji hayo, mtuhumiwa anadaiwa alivuta bangi nyingi na dawa za kulevya ambazo hatujafahamu ni aina gani…tunaendelea na uchunguzi,”alisema.
Kamanda Mambosasa alisema kutokana na hali hiyo, wamelazimika kumpeleka mtuhumiwa huyo katika Hospitali ya Mirembe iliyopo Dodoma ili aweze kupimwa akili.
Tukio hilo ni mwendelezo wa matukio ya mauaji ambayo yamekuwa yakitokea, ambapo hivi karibuni jijini Dar es Salaam mtumishi wa Wizara ya Fedha, Aneth Msuya (30) ambaye ni mdogo wa bilionea Erasto Msuya aliuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kigamboni.
Tukio jingine la kusikitisha, lilitokea mkoani Tanga mwanzoni mwa mwezi huu ambapo watu wanane waliuawa kwa kuchinjwa, wakiwamo watatu wa familia moja katika Mtaa wa Mleni.
Tukio hilo, lilitokea saa 7 usiku katika Kitongoji cha Kibatini, Kata ya Mzizima.
Watu hao, waliuawa baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa wamelala usiku.
Pia mauaji mengine yalitokea wilayani Sengerema mkoani Mwanza, ambako watu saba wakiwamo watano wa familia moja walichinjwa na wiki moja baadae watu wengine watatu walivamiwa na kuchinjwa wakiwa wanafanya ibada msikiti jijini humo.
Via>>Mtanzania
Social Plugin