BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana lilipitisha kwa kauli moja Sheria ya Marekebisho Mbalimbali, ambayo pamoja na mambo mengine, yamempa Jaji Mkuu mamlaka ya kuanzisha Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama Kuu.
Kwa mujibu wa muswada huo uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, adhabu kwa watakaokutwa na hatia zimeongezwa, huku mahakama hiyo ikiwekewa mazingira wezeshi ili iendeshe kesi hizo kwa haraka.
Mazingira wezeshi
Muswada huo wa sheria ambao kwa sasa utakuwa ukisubiri Rais ausaini ili iwe sheria kamili, umekusudia kuanzisha divisheni hiyo ya mahakama, ambayo itakuwa na majaji wake na watumishi wake wanaojitegemea.
“Divisheni Maalumu ya Mahakama Kuu, itakuwa na majaji pamoja na watumishi wengine, ambao wanahusika moja kwa moja na kesi za rushwa na uhujumu uchumi tu.
“Hatua hii itawezesha kesi za makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kusikilizwa kwa urahisi, ufanisi na kwa haraka,” alisema Masaju wakati alipokuwa akisoma muswada huo kabla ya kupitishwa na Bunge.
Hatua hiyo ya kuwa na majaji maalumu na wafanyakazi wake, Masaju alisema imelenga kuondoa udhaifu uliojitokeza wakati wa kushughulikia kesi za rushwa na uhujumu uchumi, kwa kuwa majaji waliokuwa wakisikiliza mashauri hayo, walikuwa hao hao wanaosikiliza mashauri mengine ya jinai, madai, katiba na mengine yanayofunguliwa Mahakama Kuu.
Kwa mujibu wa Masaju, hali hiyo ilisababisha uendeshaji wa kesi za rushwa na uhujumu uchumi, kutokuwa na tofauti na uendeshaji na usikilizwaji wa kesi zingine.
Mazingira mengine wezeshi yanayotengenezwa na sheria hiyo kwa divisheni hiyo, ni thamani ya fedha inayohusishwa na makosa hayo, kuwa inaanzia Sh bilioni moja.
“Inapendekezwa kuwa pale makosa ya rushwa na uhujumu uchumi yanapohusisha thamani ya fedha, basi makosa yatakayofunguliwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, yawe ni yale ambayo thamani yake haipungui Sh bilioni moja,” alisema Masaju.
Lengo la kuweka thamani hiyo ya fedha, limeelezwa kuwa ni kuiwezesha divisheni hiyo kujikita kusikiliza makosa makubwa ya rushwa na uhujumu uchumi, ili makosa madogo yasiyofikia thamani hiyo, yasikilizwe na mahakama za wilaya, mahakama za hakimu mkazi na Mahakama Kuu.
Thamani hiyo ya fedha, imetajwa pia kusaidia kuharakisha usikilizwaji wa makosa hayo bila kuathiri ufanisi na kupunguza msongamano wa mashauri katika divisheni hiyo.
Hata hivyo, divisheni hiyo pia kwa mujibu wa sheria hiyo itasikiliza makosa mengine ya rushwa na uhujumu uchumi bila kujali thamani ya fedha, kutokana na namna makosa hayo yalivyotendeka, asili yake na ugumu wa kuyawekea thamani ya fedha.
Pia Mkurugenzi wa Mashitaka amepewa mamlaka ya kutoa hati ambayo itataka mashauri mengine yatakayofunguliwa, yasikilizwe katika divisheni hiyo kwa maslahi ya umma.
Kifungo, utaifishaji mali
“Marekebisho mengine yanayopendekezwa… ni kwamba makosa ya rushwa na uhujumu uchumi chini ya sheria hii iwe ni kifungo cha gerezani, kisichopungua miaka 20 na kisichozidi miaka 30 au vyote kwa pamoja na hatua nyingine za kijinai, ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zilizopatikana kutokana na makosa hayo,” alisema Masaju wakati akiwasilisha muswada huo.
Kifungo hicho kimeongezwa kutoka katika sheria ya sasa ambayo ndiyo inayorekebishwa, ambayo ilitaka kifungo kisizidi miaka 15.
Kwa mujibu wa Masaju, maneno hayo “kifungo kisichozidi miaka 15”, yaliipa Mahakama mamlaka ya kutoa adhabu ndogo zaidi, ilimradi tu adhabu hiyo haizidi miaka 15, jambo lililoonekana kuwa baadhi ya adhabu zilikuwa ndogo kuliko uzito wa makosa.
Katika kutaifisha mali za waliokutwa na hatia, sheria hiyo imeweka masharti ya kuzuia kutumika kwa sheria zinazohusu ufilisi au uamuzi wa kufilisi kampuni, kwa mali ambayo inachunguzwa chini ya Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi.
“Marekebisho hayo yanalenga kukabili vitendo vya watu au kampuni kujifilisisha wakati uchunguzi unapoanza dhidi yao na pia kuhakikisha kuwa mali zote zinazohusika na kosa linalochunguzwa, au linaloendelea mahakamani, inaendelea kuwepo hadi uchunguzi au kesi husika itakapohitimishwa,” alisema Masaju.
Hatua hiyo imetajwa kuwa na nia ya kuiwezesha serikali kutaifisha mali hiyo, wakati kesi husika itakapokamilika na ikathibitika kuwa ina uhusiano na kosa la rushwa na uhujumu uchumi lililothibitishwa mahakamani.
“Kwa ujumla hatua hii ni njia mojawapo ya kuwafanya watu waogope kutenda makosa ya rushwa na uhujumu uchumi na pia kuhakikisha kuwa mhalifu, hanufaiki na uhalifu alioutenda kwa kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa, ufisadi na uhujumu uchumi,” alisema.
Ulinzi wa mashahidi
Marekebisho mengine yaliyoingia katika sheria hiyo, yanahusu ulinzi wa mashahidi, ambapo Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), kwa kushauriana na Mkurugenzi wa Mashitaka, wanatakiwa kuweka utaratibu wa kuhakikisha usalama wa shahidi pamoja na familia yake.
Lengo ni kusaidia usalama wa mashahidi wa kesi hizo, ili mashahidi wawezeshwe kutoa ushahidi wao bila woga, kwa kuwa kesi hizo zinahusisha watu wenye fedha na makosa yanayofanyika ni ya kupanga.
Maoni ya wabunge
Akichangia maoni yake kuhusu muswada wa sheria hiyo, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe, alisema tangu amekaa bungeni, hajawahi kuona majadiliano ya kina kwenye kamati kati ya Kamati ya Bunge na serikali ambayo yalidumu kwa wiki mbili.
Wabunge wengine, akiwemo Hussein Bashe wa Nzega Mjini (CCM), Mbunge wa Ileje, Janet Mbene (CCM), Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) na Mbunge wa Muheza, Adadi Rajab (CCM), walitaka Serikali kuiwezesha mahakama hiyo kimafunzo na kifedha, ili itekeleze wajibu wake.
Social Plugin