Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Chadema Watangaza Kuanza Ziara Nchi Nzima Kuishtaki Serikali kwa Wananchi,Ratiba Iko Hapa


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuanza ziara ya kuishtaki Serikali kwa wananchi kuhusiana na utumbuaji majipu usiofuata maadili ya kazi na kutoonyeshwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya vikao vya Bunge.


Mratibu wa ziara hiyo, Singo Benson alisema ziara itaanza Juni 7 katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na kuendelea mikoa mingine, lengo ni kuelimisha wananchi juu ya ubakwaji wa demokrasia.


“Wananchi wananyimwa haki ya msingi ya kutoona matangazo ya Bunge moja kwa moja na hakuna sababu ya msingi iliyotolewa, hivyo lazima tuwaelimishe na tuwatetee wananchi haki zao,” alisema Benson.


Aliongeza kuwa katika utumbuaji majipu unaofanyika, umekuwa kwa asilimia kubwa ukilenga majipu madogo (viongozi wa chini) na kuacha viongozi wakubwa mafisadi bila kuchukuliwa hatua yoyote.


Benson alitoa mfano wa ubakwaji wa demokrasia akisema ni kitendo cha Serikali kuingilia mihimili mingine, Bunge na Mahakama, ambapo kwa Bunge Serikali ina daiwa kuingilia uchaguzi wa mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC) ambaye anatakiwa kutoka kambi ya upinzani.


Alisema ziara hiyo itakayojumuisha Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji itakuwa na awamu nne nchi nzima huku wabunge wote na wajumbe wakuu wa chama watashiriki, akiwamo aliyekuwa mgombea urais 2015, Edward Lowassa.


Awamu ya kwanza itakayochukua siku 14 itaendelea kwa kugawana maeneo na kundi moja la viongozi wa Chadema litaenda maeneo ya Chato, Katoro, Busanda, Biharamulo, Muleba, Bukoba Mjini, Karagwe, Ngara na Geita; Kundi la pili Shinyanga mjini, Meatu, Maswa, Bariadi, Lamadi, Musoma Mjini, Bunda, Tarime na kuhitimisha Mwanza Mjini.


Benson ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uratibu na Mafunzo wa Chadema, alieleza kuwa awamu ya pili itahusisha nyanda za juu kusini na kati, awamu ya tatu itakuwa mikoa ya kaskazini na kusini na kuhitimisha jijini Dar es Salaam.


“Ziara hizi zinawakaribishwa wabunge na wanasiasa wa vyama vyote wenye lengo la kutetea haki za wananchi kwa viongozi waliowachagua,” alieleza Benson.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com