Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amekwenda Marekani na kesho ataiambia jumuiya ya kimataifa, kilichojiri kwenye Uchaguzi Mkuu na kusababisha chama chake kususia uchaguzi wa marudio wa Rais wa Zanzibar ulioipa CCM ushindi.
Mkutano huo umeandaliwa na Kituo cha Elimu ya Kimkakati na Kimataifa cha Marekani (CSIS) na utafanyika makao makuu ya taasisi hiyo yaliyoko Washington DC kuanzia saa 4:00 asubuhi.
“Tumewambia Wazanzibari kuwa ni lazima tudai haki yao ya maamuzi ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba 2015 kupitia kura zao.
"Tumewaambia tutadai haki yao ndani ya Zanzibar, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na katika jumuiya ya kimataifa,” alisema Maalim wakati akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Katika barua ya mwaliko iliyoandikwa na mkurugenzi wa CSIS, Jennifer Cooke, Maalim Seif atatoa mada kwenye mjadala uliopewa jina la “The Zanzibar Elections: Democracy Deferred (Chaguzi za Zanzibar: Demokrasia iliyocheleweshwa)”.
Maalim atakuwa miongoni mwa watoa mada watatu. Wengine ni balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania,Mark Green na naibu mkurugenzi wa kanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika wa Taasisi ya Taifa ya Kidemokrasia (NDI), Mercedeh Momeni.
“Tafadhali jiunge nasi katika kikao hiki, ambacho Bwana Hamad atachangia mtazamo wake kuhusu uchaguzi wa 2015 na ni jinsi gani Zanzibar na Tanzania zinaweza kutatua migogoro ya kikatiba na kisiasa yanayosababishwa (na mambo hayo),” inasema tovuti ya CSIS ikizungumzia mjadala huo wa kesho.
Maalim Seif alikuwa mgombea urais wa Zanzibar mwenye upinzani mkubwa kwa mgombea wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein na ameshagombea urais kwenye chaguzi zote tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992.
Mara zote amekuwa akilalamikia kuchezewa rafu na mwaka jana mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kufuta matokeo ya urais, wawakilishi na madiwani kwa maelezo kuwa sheria na kanuni za uchaguzi zilikiukwa.
Jecha alifanya uamuzi huo Oktoba 28, siku ambayo alitakiwa atangaza mshindi wa kiti cha urais baada ya matokeo ya majimbo 31 kuwa yameshatangazwa na mengine tisa yaliyosalia kuwa yameshahakikiwa.
Kabla ya kutangaza uamuzi huo, hakuonekana Oktoba 27 na siku iliyofuata alitangaza kufuta matokeo akiwa studio za kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, CUF haikushiriki na imeshatangaza kutoitambua Serikali ya Dk Shein.
Maalim Seif aliondoka juzi jioni akiwa ameambatana na mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, na katibu wake, Issa Kheir Hussein.
Kadhalika taarifa kutoka CSIS zinasema mkutano huo utashirikisha viongozi mashuhuri duniani, wakiwamo wa viongozi wa Ivory Coast na Sierra Leone.
NDI imeeleza kuwa wamemwalika Rais Alessane Watarra wa Siera Leone ili kutoa ushuhuda wa namna demokrasia ilivyoporwa katika nchi yake kabla vyombo vya kimataifa na umma kutumika na kuwaondoa madarakani viongozi waliokuwa madarakani.
Mkutano huo unafanyika wakati ambao wakuu wa NDI wamemwandikia Rais Barack Obama wa Marekani wakimlaumu kwa kuacha mambo yaendelee kama yalivyo nchini Tanzania.
Barua kwenda kwa Obama inasema Rais huyo wa taifa kubwa duniani ameshindwa kusimamia demokrasia barani Afrika, kutofanya maamuzi ya haraka dhidi ya kile kilichojiri Tanzania katika uchaguzi wa mwaka 2015.
“Tanzania imepoteza sifa yake ya kuwa kipimo cha demokrasia na utawala bora miongoni mwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati,” inasema barua hiyo ya NDI iliyoandikwa na Cooke.
“Vipi uhusiano wa Marekani uendelee wakati tunajua Tanzania ilipoteza sifa yake ya kutekeleza demokrasia? Na vipi tuweke mazingira ya kusaidia sehemu ambayo demokrasia imeporwa na maamuzi ya watu wa Zanzibar hayakuheshimiwa?”
Social Plugin