Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Kubenea Ahojiwa na Kamati ya Bunge, Maadili na Madaraka



Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ameongozana na mawakili wawili akiwamo Mbunge wa Simanjiro, James Ole Milya (Chadema) kwenda kuhojiwa kwenye Kamati ya Bunge, Maadili na Madaraka inayoongozwa na George Mkuchika.




Kubenea alihojiwa kwa zaidi ya saa moja kwa tuhuma za kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Waziri wake, Dk Hussein Mwinyi kwenye ugawaji wa ardhi kwa Kampuni ya Henan Guiji Industry.


Mbunge huyo alifikishwa mbele ya kamati hiyo Alhamis iliyopita ili kujibu mashtaka hayo baada ya Dk Mwinyi kulalamika wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17.


Dk Mwinyi aliliambia Bunge wakati akihitimisha bajeti ya wizara hiyo kuwa yuko tayari kujiuzulu uwaziri iwapo Kubenea atathibitisha tuhuma hizo mbele ya Bunge.


Kufuatia ombi hilo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alimwagiza Kubenea kupeleka uthibitisho katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ukachunguzwe.



“Waheshimiwa wabunge pamoja na ombi hilo la mheshimiwa waziri, lakini pia ameleta malalamiko rasmi kwa Spika akiomba tuhuma zilizoelekezwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na dhidi yake binafsi zifanyiwe uchunguzi na kumtaka mheshimiwa Kubenea athibitishe na kama atashindwa achukuliwe hatua stahiki,” alisema Dk Tulia.


Awali, wakati akichangia bajeti hiyo, mbunge huyo alisema kampuni hiyo ambayo inataka kuingia mkataba na JWTZ, inajifunga mkataba mwingine na Dk Mwinyi na huenda ukawa umesainiwa na au haujasainiwa.


Hata hivyo, Kubenea na wabunge wengine wa kambi ya upinzani wamesusia vikao vya Bunge vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa madai kuwa hawatendei haki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com