WATU watano wamefariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa katika ajali ya basi lenye namba za usajili T. 449 BCB mali ya kampuni ya Super Sami lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamikia leo katika eneo la Bashini Kata ya Mabuki Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, baada ya gari hilo kugonga jiwe lililokuwa barabarani na kusababisha William Elias, Dereva wa gari hilo kushindwa kulimdu.
Watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Valieth Odede, William Elias (Dereva) huku mwanaume mmoja na wanawake wawili wenye umri wa miaka 25- 30 majina yao bado yakiwa bado hayajafahamika mpaka hivi sasa.
Majeruhi katika ajali hiyo ni 13, ambao ni Sophia Miraji, Kibilo Mwacha, Boniphace Charles na Frank Kunyumi ambao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya awali kutokana na kujeruhiwa vibaya.
Wengine ni Stanley Zacharia, Sia Dauson, Hellen Leheke, Michael Leonard, Kudra Ibrahim (mtoto wa miaka miwili), Zamda Issa, Marieth Christopher, Elizabeth Simon na Dickson Msamba ambao wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) jijini hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, akizungumzia tukio hilo, amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari hilo kuwa katika mwendo kasi na kusababisha ashindwe kulimdu basi hilo na kusababisha kupinduka.
Msangi, amesema kuwa kutokana na ajali hiyo jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea kuchunguza gari hilo pamoja na kufanya uchunguzi juu ya ajali hiyo iliosababisha vifo vya watu watano kupoteza maisha na wengine 13 kujeruhiwa.