Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Majambazi Yazua Hofu Mwanza,Wananchi Waanza Kuhama Makazi yao


Siku moja baada ya kutokea mapambano ya zaidi ya saa 16 baina ya Jeshi la Polisi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kwenye mapango ya mlima ya Utemini, wananchi wa eneo hilo wameingiwa na hofu ya usalama wao baada ya baadhi yao kuona wahalifu wakitoroka wakati wa tukio hilo.


Wananchi hao wana hofu kuwa majambazi waliotoroka wanaweza kurejea na kuwadhuru na tayari baadhi wameanza kuhama makazi yao.


Hofu ya wananchi hao imekuja baada ya polisi kupambana na watu hao usiku wa kuamkia juzi, wakitumia silaha kali zilizo sababisha kizaazaa kwa wakazi wa Utemini, kutokana na milio ya risasi na mabomu.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Utemini Ibanda, kata ya Mkolani, Jukael Kiula jana alisema baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na mapango hayo wameanza kuhama makazi yao wakihofia kurejea kwa majambazi hao.


“Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya majirani, walikuwa wakiwaona watu wakipanda na kushuka kutoka kwenye milima yenye mapango waliyojificha watu hao. Lakini hawakuwatilia shaka wakidhani ni watu wanaopasua mawe, hadi siku polisi walipopambana na majambazi hayo,” alisema Kiula.


Mwenyekiti huyo aliiomba Serikali kuimarisha ulinzi na doria kwenye mtaa huo ili kuwahakikishia usalama wananchi.


“Hata ikibidi, askari wa Jeshi la Wananchi waweke kambi ya muda kwenye eneo hilo kudhibiti vitendo vyovyote vya uvamizi,”alisema.


Akizungumza na wakazi wa Utemini jana, mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga aliwahakikishia kuwa Serikali itaimarisha ulinzi kudhibiti uwezekano wa wahalifu kuendelea kutumia mapango hayo kujificha.


Konisaga ambaye alitembelea eneo la tukio jana, aliwaomba wakazi kutoa taarifa za maficho ya wahalifu pale wanapohisi kuna nyendo zinazotilia shaka.


Kamanda wa polisi wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema kiama cha wahalifu kimefika na kwamba tayari vyombo vya dola vimebaini mitandao ya uhalifu na wahusika na itawasaka usiku na mchana.


“Hatutakuwa na msalie mtume katika mapambano dhidi ya ujambazi Mwanza. Wote wanaojihusha na ujambazi watambue kuwa yatawakuta yaliyowakuta wenzao waliojaribu kupambana na polisi,” alionya Kamanda Msangi.


Mkuu wa Mkoa, John Mongella alisema mkakati wa kuifanya Mwanzaa iwe salama umeanza na hakuna mhalifu atakayeingia Mwanza na kutoka salama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com