Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan leo hii amezindua jukwaa la kuwezesha wanawake na akaunti maalum ya mikopo ya MALAIKA inayolenga kuwawezesha wanawake wa hali ya chini kiuchumi kupitia Benki ya wanawake katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Akiongea katika uzinduzi huo Mheshimiwa Samia Suluhu amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni kuwapa uwezo wanawake waweze kutoka katika sekta isiyo rasmi na kuingia katika sekta rasmi na hivyo kuwainua kiuchumi kwani mchango wa mwanamke mpaka sasa bado haujaongezeka thamani.
Aidha Bi Samia ameagiza kuwa kuanzia sasa asilimia 35% ya tenda za serikali za mitaa ziende kwa wanawake na vijana ili kuwawezesha kiuchumi na kuwataka wanawake kubadilika kifikra na hata wanapopata mikopo hii wawe na nidhamu katika matumizi yake.
Hata hivyo Mhe. Suluhu ametoa rai kwa mabenki kufikisha huduma zao vijijini ili huduma ya mikopo iwafikie wanawake wachangie uchumi wa dunia na sio tu kwa familia huku akiwahimiza wanawake kupendana,kushirikiana na kusaidiana.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Watoto na Wazee Dkt.Hamisi Kigwangala amesema kuwa serikali imeendelea kusaidia wanawake katika Nyanja mbalimbali ikiwemo kuweka usawa wa jinsia kwa wanawake kiuchumi ,kutoa vikwazo katika masoko na kuondoa mila kandamizi.
Aidha Dkt Kigwangala ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara kwa wanawake kwa kufanya mafunzo ya ujasiliamali na kuweka sera nzuri ambayo yote haya yameainishwa katika ilani ya chama cha mapinduzi ya 2015-2020 uku akieleza mafanikio makubwa ya benki ya wanawake ambayo mpaka sasa imetoa mikopo yenye thamani ya bilioni 86.
Uzinduzi wa Jukwaa hilo na akaunti ya MALAIKA ya mikopo uliendana na mada mbalimbali kutoka kwa wadau mbalimbali kama Crdb,Benki ya wanawake,Nssf ,Wizara ya Viwanda na Biashara na Tcra.