Picha!! Rais Magufuli Amuapisha Jaji Wa Mahakama Ya Rufani Na Jaji Kiongozi,Aagana Na Balozi Wa Oman


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Juni, 2016 amemuapisha Mhe. Jaji Shaaban Ali Lila kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Ikulu Jijini Dar es salaam.

Kabla ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Jaji Shaaban Ali Lila alikuwa Jaji Kiongozi.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Jaji Ferdinand Leons Katipwa Wambali kuwa Jaji Kiongozi.

Kabla ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Jaji Kiongozi, Mhe. Jaji Ferdinand Leons Katipwa Wambali alikuwa Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mkoani Tanga.

Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Leons Katipwa Wambali amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Jaji Shaaban Ali Lila ambaye amekua Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagana na Balozi wa Oman hapa nchini Mhe. Saoud Ali Mohamed al Ruqaishi ambaye amemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

Akizungumza na Balozi huyo, Ikulu Jijini Dar es salaam Rais Magufuli ameishukuru Oman kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano wa kihistoria na kidugu na Tanzania, na ameahidi kuwa serikali yake ya awamu ya tano ipo tayari kuongeza ushirikiano huo.

Mhe. Rais Magufuli pia amemuomba Balozi Saoud Ali Mohamed al Ruqaishi kufikisha salamu zake kwa Sultani wa Oman Mtukufu Qaboos bin Said al Said na kumueleza kuwa Tanzania inawakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Oman na inatarajia kuona miradi ya ushirikiano katika uwekezaji ukiwemo mradi wa Bagamoyo inaanza kutekelezwa haraka.

"Naomba umfikishie salamu zangu za dhati Mtukufu Qaboos bin Said al Said, Sultan wa Oman na umwambie tunamkaribisha Tanzania na nitafurahi kuona mradi wa uwekezaji wa Bagamoyo unakuwa kielezo cha undugu na urafiki wetu uliodumu kwa miaka mingi" Amesema Rais Magufuli.

Tanzania kwa kushirikiana na nchi za Oman na China zimekubaliana kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo Mkoani Pwani.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
10 Juni, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Jaji Ferdinand Leons Katipwa Wambali kuwa Jaji Kiongozi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Jaji Shaaban Ali Lila mara baada ya kumuapisha kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Jaji Ferdinand Leons Katipwa Wambali mara baada ya kumuapisha kuwa Jaji Kiongozi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani Jaji Shaaban Ali Lila(kushoto) pamoja na Jaji Kiongozi Jaji Ferdinand Leons Katipwa Wambali (kulia)mara baada ya tukio la uapisho lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani Jaji Shaaban Ali Lila(kushoto) pamoja na Jaji kiongozi Jaji Ferdinand Leons Katipwa Wambali, wengine katika picha ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Jaji mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othmani mara baada ya tukio la uapisho wa Majaji hao Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani Jaji Shaaban Ali Lila(kushoto) pamoja na Jaji kiongozi Jaji Ferdinand Leons Katipwa Wambali, wengine katika picha ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Jaji mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othmani pamoja na Majaji mbalimbali wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza kwa furaha huku akiwa amemshika mkono Jaji wa Mahakama ya Rufani Jaji Shaaban Ali Lila huku viongozi wengine wakishuhudia ikulu jijini Dar es Salaa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Balozi wa Oman hapa nchini Soud Al Ruqaishi ambaye anamaliza muda wake wa kufanya kazi hapa nchini Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Oman hapa nchini Soud Al Ruqaishi ambaye anamaliza muda wake wa kufanyakazi hapa nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Waandishi wa Habari waliofika Ikulu kwa ajili ya tukio la uapisho wa Jaji wa Mahakama ya Rufani pamoja na Jaji Kiongozi Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na IKULU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post