Picha!! Rais Magufuli Atembelea Kanisa La Maombezi La Mchungaji Antony Lusekelo ‘Mzee Wa Upako’ Jijini Dar es salaa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitembelea Kanisa la Maombezi linaloongozwa na Mchungaji Antony Lusekelo (Mzee wa Upako) lililopo Ubungo Kibangu Jijini Dar es salaam na kuwaahidi waumini wa kanisa hilo kuwa Serikali yake itatengeneza barabara ya kutoka Ubungo Kibangu hadi River Side ambako itaungana na barabara ya Mandela.


Rais Magufuli ambaye amezungumza katika ibada ya asubuhi ya Kanisa hilo iliyofanyika leo tarehe 05 Juni, 2016 amesema amepita katika barabara hiyo ambayo imekuwa ikitumiwa na waumini wa kanisa hilo na wananchi wengine wa eneo la Ubungo Kibangu kwa lengo la kujionea hali halisi.


Aidha, Rais Magufuli amempongeza Kiongozi wa Kanisa hilo Mchungaji Antony Lusekelo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako kwa huduma ya maombezi anayoitoa kwa waumini wake na watazamaji wanaofuatilia vipindi vyake vya Mahubiri kupitia Luninga.


“Mimi ni mfuatiliaji mzuri sana wa mahubiri yako, kwa hiyo mahubiri unapoyatoa yanasambaa, kwa kweli mimi na familia yangu huwa yanatubariki sana, kwa hiyo nataka kukuthibitishia ninakupenda sana.


“Ndio maana kuna siku moja, ulizungumza kuhusu shida ya barabara yako ikabidi nitafute mbinu za namna gani tunaweza kuishughulikia kwa utaratibu ulio wazi, nikamtuma meneja wa barabara wa Mkoa wa Dar es salaam, akaja, akaipitia na akafahamu changamoto zilizopo, akafanya upembuzi yakinifu na usanifu, nataka kukuthibitishia kuwa fedha za kutengenezea barabara hii zipo” Amesema Dkt. Magufuli huku akishangiliwa na waumini.


Kwa upande wake Kiongozi wa Kanisa la Maombezi Mchungaji Antony Lusekelo (Mzee wa Upako) amemshukuru Rais Magufuli kwa kulitembelea kanisa hilo, na amemuombea heri katika uongozi wake ili aweze kufanikisha azma ya kuliletea taifa maendeleo ikiwemo mpango wa kuanzisha viwanda.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
05 Juni, 2016


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post