Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Polisi Wasiowapigia Saluti Wabunge Kukatwa Mishahara,Kupigishwa Gwaride


Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Fakharia Khamis amehoji bungeni adhabu gani askari anapewa ikiwa atashindwa kutoa saluti kwa mbunge.


Katika swali la nyongeza mbunge huyo alitaka kujua maana ya saluti kwa askari ni nini, na viongozi gani wa uraiani wanaotakiwa kupigiwa saluti katika mhimili wa Bunge, Serikali na Mahakama.


Akijibu swali la mbunge huyo, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alisema Serikali imetangaza adhabu ya kuwakata mishahara na adhabu nyingine, askari polisi wote nchini ambao hawatawapigia saluti wabunge wa Bunge la Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Ole Nasha alisema kumpigia saluti mbunge ni jambo la lazima kwa askari kwa kuwa lipo kwenye moja ya masharti yao, hivyo kutokufanya hivyo ni kushindwa kutii kiapo cha uaminifu wao.


“Askari asipotoa saluti unatakiwa kumripoti kwa kiongozi wake ambapo atapewa adhabu ikiwamo kukatwa mshahara, kupigishwa paredi, kufanya usafi katika maeneo ya vituo na adhabu nyingine nyingi zinazofanana na hizo,” alisema Ole Nasha.


Alisema saluti ni salamu ya kijeshi ambayo hutolewa na askari kwa mujibu wa kanuni za kudumu za utendaji za jeshi la polisi (Police General Orders –PGO No 102).


Naibu Waziri alisema sheria hiyo imewataja askari wa vyeo vyote kuwa wanatakiwa kupiga saluti kwa Rais wa Jamhuri na Rais wa Zanzibar, Makamu wa Rais na Makamu wawili wote wa Zanzibar, majaji wakuu wa Muungano na Zanzibar.


Wengine ni Spika wa Muungano na Zanzibar, mawaziri wote wa Jamhuri na Zanzibar, makatibu wa Bunge na Baraza la Wawakilishi, wabunge wa muungano na wawakilishi wanapokuwa kwenye maeneo yao, wakuu wa mikoa, majaji wanapokuwa kwenye maeneo yao na kwa nafasi zingine ni wakuu wa wilaya na mahakimu kwenye maeneo yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com