JESHI la majini la Marekani limepiga marufuku unywaji wa pombe kwa wanamaji wote walioko Japan pamoja na kutotoka nje ya kambi zao.
Hatua hiyo imechukuliwa siku moja tu baada ya mwanajeshi Mmarekani kukamatwa na maofisa wa polisi nchini Japan kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa katika Kisiwa cha Okinawa.
Mwanajeshi huyo, Aimee Mejia (21) alihusika katika ajali tatu tofauti katika kisiwa hicho na kuwajeruhi vibaya watu wawili.
Mejia alikuwa akiendesha upande usiofaa wa barabara na akagonga mwanamke mmoja.
Maofisa watakaoruhusiwa kutoka nje ya kambi ni wale tu watakaopewa vibali maalumu au watakaokuwa wanatekeleza majukumu muhimu kama ya jeshi au kifamilia.
Jeshi la Marekani tayari lilikuwa katika kashfa baada ya mfanyakazi wake kubaka na kisha kumuua mwanamke Mjapani.
Marekani ina takriban wanamaji 50,000 nchini Japan na 19,000 katika kisiwa hicho na kwa muda sasa wamekuwa wanakabiliwa na shinikizo waondoke kutoka kwa wenyeji.
Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe alieleza kukasirishwa kwake na tukio hilo na aliliibua wakati wa mkutano wa mataifa saba tajiri (G7) na Rais wa Marekani, Barack Obama hivi karibuni.
Social Plugin