Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Rais Magufuli Aeleza Kwa Kina Sababu Za Kusitisha Ajira Serikalini


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali imeamua kusimamisha kwa muda mfupi usiozidi miezi miwili zoezi la utoaji ajira mpya na upandishaji wa vyeo kwa watumishi wa umma kwa lengo la kupisha uhakiki wa watumishi wa umma katika orodha ya malipo ya mshahara na kuondoa watumishi hewa.

Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 22 Juni, 2016 katika Jubilei ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) iliyofanyika katika ukumbi wa Benki hiyo, Mtaa wa Mirambo Jijini Dar es salaam.

Dkt. Magufuli amesema zoezi hilo halina nia ya kuwakatisha tamaa watumishi wa umma na amewahakikishia watumishi wote wa umma kuwa serikali itaendelea kuajiri watumishi wapya na kuwapandisha vyeo waliopo kama kawaida mara baada ya kukamilika kwa zoezi.

"Serikali ninayoiongoza haina nia ya kuwakatisha tamaa wafanyakazi, lengo lake ni kujipanga kwa makosa tuliyoyafanya, na ndio maana nimesema kwa kipindi cha mwezi mmoja hivi au hata mwezi mmoja na nusu, haitazidi miezi miwili, tusiajiri mtumishi yeyote serikalini, lakini pia katika kipindi cha mwezi mmoja hatutawapandisha vyeo wafanyakazi, ninaomba wafanyakazi waelewe hili, kwa sababu tukiendelea tutakuwa tunawapandisha vyeo hata wafanyakazi ambao hawapo, tunafanya ukaguzi wote tukishamaliza wafanyakazi wataendelea kupandishwa vyeo" amesema Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kazi kubwa iliyoifanya katika kipindi cha miaka 50 katika kusimamia sekta ya fedha na maendeleo, lakini ameitaka benki hiyo kuchukua hatua za haraka dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoyahusu majukumu yake.

Miongoni mwa changamoto hizo ni idadi ndogo ya watanzania wanaonufaika na huduma za benki hususani waishio vijijini, benki kutoza riba kubwa na hivyo kusababisha wananchi kuogopa kukopa kwa hofu ya kushindwa kulipa, kuilinda thamani ya Shilingi ya Tanzania, na kukusanya kodi ipasavyo kwa miamala inayofanywa kupitia simu za mkononi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Changamoto nyingine ni kusimamia ipasavyo maduka ya kubadilishia fedha (Bureau de change) ili kuthibiti utakatishaji na utoroshaji wa fedha na kuhakikisha ushukaji wa mfumuko wa bei uliotoka asilimia 28 hadi kufikia asilimia 5.1 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita unaonesha matokeo katika nafuu ya maisha ya watanzania.

Aidha, Rais Magufuli ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuchukua hatua mara moja dhidi ya benki ambazo hazizalishi faida zikiwemo benki za serikali, kufuta account mfu (Domant account) na kuanzisha mara moja akaunti moja ya mapato na matumizi ya serikali (Single Treasury Account)

Jubilei hiyo imehudhuriwa na Magavana na Manaibu Gavana kutoka nchi 18 za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa Taasisi za fedha za Afrika na Makatibu wakuu wa Wizara za Fedha na Mipango wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
22 Juni, 2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com