Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi Ataka Mabasi ya Mwendo Kasi kwa Ajili ya Wanafunzi na Watalii

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ameishauri Kampuni inayoendesha Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (UDART) kuongeza mabasi ya wanafunzi na mengine ya wazi juu ya watalii wanaoitembelea nchini ili waweze kuangalia mandhari ya jijini Dar es Salaam.


Rais Mwinyi alitoa ushauri huo jana alipotembelea mradi huo akiwa na mkewe, Sitti Mwinyi na kupokewa na Kaimu Mtendaji mkuu wake, Ronald Lwakatale, Mtendaji wa kampuni inayoendesha mradi huo, David Mgwassa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi.


Mwinyi alikata tiketi katika Kituo cha Morocco na kupanda gari kwenda Kariakoo, Gerezani kisha Kivukoni.


Alipofika katika kituo hicho alikutana na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mtendani na kuzungumza nao kwa kifupi kisha kuwaeleza ushauri huo alioutoa kwa UDART.


“Nimekuja kupata maarifa na kuona mabasi yetu mapya yanavyofanya kazi kuhudumia wana Dar es Salaam.


"Wakati nipo kwenye basi nimeteta na viongozi nikiwashauri kama kuna uwezekanao wa kuwa na basi moja au mawili ya wazi ambayo unaweza kupanda juu ili kuona mazingira ya jiji vizuri,” alisema Mwinyi,


Alisema magari hayo ya wazi yatawasaidia watalii kulitazama jiji vizuri, lakini pia wanafunzi kujionea mandhari yake na kujifunza.


Mtendaji wa UDART, David Mgwassa alisema elimu imeanza kuwaingia wananchi kwani usumbufu na ajali hakuna na kwamba wiki ijayo matumizi ya kadi yataanza baada ya hatua za awali kukamilika na kubakia vitu vichache.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com