Serikali: Kuna Upungufu Wa Walimu 22,460 wa Sayansi na Hisabati Katika shule za Sekondari Tanzania

Serikali imesema kuna upungufu wa walimu 22,460 wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule sekondari na kuna ziada ya walimu 7,988 wa masomo ya sana,Lugha na Biashara ambapo kwa mwaka 2015/2016 serikali inatarajia kuajiri walimu 35,411 kwa shule za msingi na sekondari ili kuongeza idadi ya walimu. 
 
 
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa Prof.Joyce Ndalichako wakati akijibu swali la Mheshimiwa Kasuku Samsoni Bilago Mbunge wa Buyungu aliyetaka kujua serikali inawalimu wangapi wa sekondari. 
 

Akijibu swali hilo Mheshimiwa Ndalichako amesema idadi hiyo ikishaongezwa ni wazi kuwa itasaidia kupunguza mzigo mkubwa ulipo kwa walimu ambao umekuwa ukipigwa kelele kila mara na hivyo kugeuka kuwa ni kero kubwa. 
 

Ameongeza kuwa lengo la kuongeza walimu hao ni kuongeza tija katika sekta ya elimu ambayo ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa lolote. 
 

Mheshimiwa Ndalichako akasema takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya walimu waliopo ni 88,999 kati ya walimu 18,545 ni wa masomo ya sayansi na hisabati na walimu 70,454 ni masomo ya lugha sanaa na biashara. 
 

Aidha ameongeza kuwa serikali kupitia halmashauri za wilaya,miji, manispaa ya majiji imeendelea kutenga fedha katika bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari kwa lengo la kupunguza changamoto ya utoshelevu wa miundombinu kama vile nyumba vya madarasa na nyumba za walimu. 
 

Aidha Mheshimiwa Ndalichako akongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2015/6 serikali imetenga shilingi bilioni 67.83 ambazo zimeshapokelewa katika halmashauri mbalimbali na zimetumika kwa ajili ya ukarabati,ujenzi wa nyumba za walimu na uwekaji wa umeme katika shule za sekondari 528 nchini kote. 
 

Aidha katika bajeti ya mwaka 2016/17 zimetengwa shilingi bilioni 48.3 kwa ajili ya kazi hizo.
Via>>ITV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post