Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Serikali ya Tanzania Kununua Ndege Tatu na Meli Moja kuboresha Usafiri Katika Maziwa Makuu


Serikali imejipanga kununua ndege tatu na meli moja kwa ajili ya kuboresha usafiri wa anga na majini katika maziwa makuu kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.


Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Philip Mpango wakati akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17.


“Serikali itanunua meli moja mpya ya usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria na ukarabati wa meli za MV Victoria, MV Butiama na MV Liemba na kuimarisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ikijumuisha ununuzi wa ndege 3 mpya” alisema Waziri Mpango.


Alisema miongoni mwa ndege hizo kuwa ni Bombardier CS300 yenye uwezo wa kubeba abiria 100 – 150 na ndege mbili Bombardier Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 67- 88 kila moja.


Aidha, Waziri Mpango alisema kuwa Serikali imeweka mikakati ya kujenga na kuboresha miundombinu wezeshi, kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, kuhamasisha ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma.

Kwa mujibu wa Mpangpo Ili kuhakikisha utekelezaji huo unafanikiwa Serikali imeweka jitihada mahususi za kuongeza kasi ya kulipa fidia katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZs na SEZs); Benki ya Rasilimali kuongeza utoaji wa mikopo katika sekta mbali mbali kutoka shilingi bilioni 538.7 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 726.9 kwa mwaka 2016.


Aliongeza kuwa jitihada nyingine ni pamoja na kuitangaza Benki ya Maendeleo ya Kilimo na huduma zake ili wananchi waweze kutumia fursa za mikopo zinazopatikana katika benki hiyo na kuwezesha Kituo cha Uwekezaji Tanzania kuwa na ardhi yenye hatimiliki kwa ajili ya kuikodisha kwa wawekezaji wa nje.


Kwa mujibu wa Waziri Mpango miradi mingi mikubwa itatekelezwa kwa ubia. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Biashara na Huduma Kurasini, miradi ya Chuma-Liganga na makaa ya mawe – Mchuchuma na Mradi wa barabara wa Dar es Salaam – Chalinze- Morogoro Express Way.


Waziri Mpango alisema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi ambayo ilishaanzishwa ikiwa ni pamoja na nishati ukiwemo mradi wa Liquified Natural Gas, kilimo cha mazao, mifugo, uvuvi, misitu, maji na miundombinu ya reli na barabara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com