Serikali Yatangaza Vita Dhidi ya Majambazi na Wauaji


Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni ametangaza vita dhidi ya majambazi na watu wanaojihusha na mauaji.


Alisema Serikali imelazimika kutangaza vita hivyo baada ya kutokea matukio 41 yaliyohusisha mauaji ya kinyama tangu Januari hadi mwezi uliopita.


“Serikali ipo kazini, sasa inatangaza vita dhidi ya watu wanaojihusisha na ujambazi, watakaobainika hakika wataangamizwa hatuwezi kukubali watu wazidi kupoteza maisha pasipo na sababu za msingi,” alisema Masauni.


Waziri huyo alitembelea Msikiti wa Rahman Mtaa wa Utemini Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, Mwanza na kusema matukio hayo yanapaswa kutokomezwa na kukemewa kwa nguvu zote.


“Mauaji hayo yalikuwa ya kutisha hivyo ilikuwa ni lazima watuhumiwa wakamatwe, hata hao waliokimbia wanapaswa kutiwa mbaroni,” alisema.


Pia, alionya tabia ya baadhi ya polisi kujihusha na vitendo vya uhalifu na kupoteza imani na uaminifu kwa wananchi.


Aliwataka polisi wanaofanya vitendo hivyo kuacha na badala yake wapambane na wahalifu.


Masauni alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa utulivu, hivyo haitakubali watu wachache kuvuruga amani iliyopo


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema vyombo vya usalama vipo imara kwani baadhi ya wahalifu wameuawa na wengine kukamatwa na wanaendelea kuhojiwa.


Mjumbe wa baraza la masheikh Wilaya ya Nyamagana, Saidi Darwesh alisema tukio la mauaji ya msikitini limesababisha hofu kwa waumini, hususan kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kwani wengine hawaendi msikitini kuswali.


Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Utemini, Jukael Kiula alisema wakazi wa Kata ya Mkolani wamejitolea kujenga kituo cha polisi katika mtaa huo ili kudhibiti uhalifu unaotokea mara kwa mara.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wa pili kushoto) akimuuliza jambo Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi (kushoto) wakati walipokuwa wanawasili msikiti wa Rahmani mkoani humo uliovamiwa na majambazi na kuua waumini watatu ndani ya msikini huo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wa pili kulia) akimsikiliza Mkuu wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Ahmed Msangi (kulia) wakati walipokuwa wanatoka msikitini mara baada ya kuzungumza na waumini wa msikiti huo wa Rahmani mkoani humo. Msikiti huo ulivamiwa na majambazi hivi karinbuni na watu watatu waliuawa. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mzee wa Msikiti wa Rahmani uliopo Mkolani, jijini Mwanza, Abeid Gati (kushoto), akimpa fedha mke wa mmoja wa watu waliouawa na majambazi ndani ya msikiti huo. Fedha hizo zilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (aliyevaa Kaunda suti) ikiwa ni rambirambi yake kwa wafiwa wote watatu ambao walipoteza wenza wao katika mauaji hayo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (kushoto) akimpa pole askari Polisi, Mageni Kaseha aliyepigwa risasi ya mguu na majambazi wakati wa mapambano kati ya polisi na majamabazi hao katika mapango ya utemini, jijini Mwanza. Askari huyo amelazwa katika Zahanati ya Jeshi hilo iliyopo katika Kambi ya Mabatini, jijini humo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post