Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Sheria ya Mahakama ya Mafisadi Yatua Rasmi Bungeni,Hatia ya Rushwa au Uhujumu Uchumi Jela Miaka 30


Serikali imewasilisha miswada miwili ya marekebisho ya sheria mbalimbali ya mwaka 2016 ikiwamo ya kuanzishwa kwa Mahakama Maalumu ya Rushwa.


Watakaokutwa na hatia ya makosa ya rushwa au uhujumu uchumi, watafungwa kifungo kisichopungua miaka 20 na kisichozidi miaka 30.


Kuanzishwa kwa mahakama hiyo ni kutimiza ilani ya CCM na ahadi ya Rais John Magufuli kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana kuwa ataianzisha ili kushughulika na mafisadi pamoja na wahujumu uchumi.


Kwa mujibu wa muswada huo, mahakama hiyo inaanzishwa katika marekebisho ya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 yatakayo fanyika katika Kifungu cha 3.


“Lengo la marekebisho hayo ni kuanzisha Divisheni ya Mahakama Kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi itakayokuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri yanayohusiana na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, ambayo itakuwa na mamlaka ya kusikiliza mashauri yenye thamani isiyopungua Sh1 bilioni,” unaeleza muswada huo uliowasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni jana.


Mbali na makosa hayo, pia mahakama hiyo itashughulika na makosa ya uhujumu uchumi bila kujali thamani yake.


Katika sheria hiyo, yatafanyika marekebisho mengine yanayohusu muundo, mamlaka na utekelezaji wa mahakama inayopendekezwa.


Pia masuala ya kuzuia ufilisi, mamlaka ya Jaji Mkuu kutengeneza kanuni na makosa ya rushwa na uhujumu uchumi, ni mambo yaliyozingatiwa katika marekebisho hayo.


Muswada huo umeeleza kuwa masharti yaliyomo kwenye Sheria ya Usalama wa Mashahidi, Sura ya 446 yanapendekezwa kutumika katika masuala yanayohusiana na usalama wa mashahidi kwa kukifanyia marekebisho kifungu cha 53.


Masuala mengine yanayopendekezwa yanahusu utaratibu wa kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, utoaji wa dhamana na adhabu, pamoja na utaratibu wa kukata rufaa.


“Taratibu nyingine za uendeshaji na utekelezaji wa masharti ya sheria hii itakuwa kama itakavyofafanuliwa katika kanuni zitakazoandaliwa na Jaji Mkuu,” umeeleza mswada huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com