TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa ufafanuzi kuhusu ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka jana, iliyowasilishwa na Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya (EU).
NEC imesisitiza kwamba ripoti hiyo imebainisha mapungufu ambayo hayapo kwenye sheria na taratibu, zinazoiongoza tume hiyo.
Miongoni mwa mapungufu waliyoyatoa waangalizi hao ni Suala la Uchaguzi wa Zanzibar, Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na haki ya wagombea binafsi kugombea nafasi katika uchaguzi wowote wa Tanzania Bara na Zanzibar, mgawanyo wa majimbo na uwazi wa kuhesabu kura.
Akitoa ufafanuzi huo, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema kuwa kwa mujibu wa sheria, waliwapa nafasi hiyo waangalizi wa ndani na nje kuangalia uchaguzi wa Tanzania Bara , kama unaenda kulingana na Katiba, sheria na taratibu za uchaguzi huo.
Alisema kuwa katika ripoti hiyo, waangalizi hao wamezungumzia uchaguzi wa Zanzibar, ambao NEC hawahusiki nao na kwamba wamefanya makosa, kwa kuwa wao walikuwa waangalizi wa uchaguzi wa Tanzania Bara na sio Zanzibar.
‘’Waangalizi wowote wa uchaguzi wanapoomba kibali kuangalia uchaguzi, wanatakiwa kufuata taratibu kwa kutambua kwamba kuna NEC na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Sisi tulitoa kibali kwa waangalizi hawa kuangalia uchaguzi wetu na sio wa Zanzibar,’’ alisema.
Aliongeza kuwa, ‘’hawakupaswa kuingiza katika ripoti yao masuala ya uchaguzi wa Zanzibar ulivyokuwa, badala yake wangeeleza kama NEC hatukufuata sheria na taratibu kwenye uchaguzi huu wa Tanzania Bara.”
Alisema pia kuwa waangalizi walitakiwa kuangalia uchaguzi huo na sio kupendekeza kwamba uchaguzi ulitakiwa kuwa vipi.
Kuhusu suala la mgombea binafsi, alisema Katiba iliyopo sasa haijaruhusu, hivyo wasingeweza kuweka wagombea hao, kwani Katiba ingewabana.
Kailima alisema kuwa endapo Katiba Inayopendekezwa ingepitishwa, waangalizi hao wangeweza kuhoji kwa nini hakukuwepo na mgombea binafsi, kwani ndiyo inaeleza kuhusu mambo hayo.
Akizungumzia mgawanyo wa majimbo, Kailima alisema kuwa kila halmashauri ya mji na wilaya ni jimbo na kwamba hawapaswi kulinganisha kati ya Halmashauri ya Temeke yenye watu 419,612 na jimbo la Madaba lenye watu 27,502, kuwa mgawanyo wake haukufuata uwiano.
Alisema kuwa mgawanyo wa majimbo, huzingatia mambo mengi, ikiwemo jiografia ya eneo lenyewe. Alieleza pia kuwa NEC haijawanyima haki Wazanzibari kwa kutoongeza idadi ya majimbo, kwa kuwa Bunge ambalo lilitakiwa kujadili, lilikuwa limekamilisha kazi yake.
Alisema kwamba ZEC yenyewe ilichelewa kutangaza mabadiliko hayo ya majimbo kutoka 50 hadi 54.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa mara ya kwanza Tanzania matokeo ya uchaguzi wa Madiwani na Wabunge yalikuwa yanabandikwa kwenye vituo vya kupigia kura pamoja na matokeo ya awali ya Rais.
Alisisitiza kuwa matokeo yote, yalikuwa yanasainiwa na wawakilishi kutoka vyama mbalimbali vya siasa na kutangazwa kwa wananchi.
Aidha, alisema kuwa hawakuweza kutangaza wabunge wa viti maalumu kabla ya uchaguzi, kwani kisheria wanachagua wagombea hao baada ya kujua idadi ya kura ya asilimia tano zilizopata chama, hivyo wasingeweza kutangaza kabla ya uchaguzi.
Hata hivyo, alisema kuwa Tume hiyo imepokea mapendekezo yao na itayafanyia kazi ikiwemo kuwa na watumishi kwa ngazi zote. Kailima alisema kuwa hali hiyo, itawasaidia kujua namna ya kuwaadhibu watumishi ambao watakiuka utaratibu wa NEC.
‘’Pia tutaongeza muda wa daftari la kupiga kura kuhakikisha kwamba kwa mwaka linakuwepo mara mbili ili wapiga kura wote waangalie. Lakini suala la Sheria ya Makosa ya Mtandao wanatakiwa kulipeleka kwa wahusika na mengine kwa serikali kwani sisi kama NEC hatuhusiki nayo,’’ alisema.
Social Plugin