Mwenyekiti mpya wa Timu ya Stand United Dkt. Ellyson Maeja akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club-SPC) leo mjini Shinyanga
******
Siku moja tu baada ya uongozi wa mpya wa timu ya Stand United (CHAMA LA WANA) kuanza kuchapa kazi baada ya kufanya uchaguzi siku ya Jumapili wiki iliyopita, uongozi wa timu hiyo umetangaza kuwaacha kuwasajili wachezaji saba kutokana baadhi yao kumaliza mkataba wao na wengine kujisajili na timu za nje.Mwandishi wa Malunde1 blog Kadama Malunde,anaripoti
Akitangaza uamuzi wa timu kwa waandishi wa habari katika ofisi ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga leo, Mwenyekiti wa klabu hiyo Dkt. Ellyson Maeja amesema uamuzi umefikiwa jana Jumatatu baada ya kikao cha kamati ya utendaji cha timu hiyo kuketi na kujadili mambo kadha wa kadha ya kujenga klabu hiyo.
Dkt. Maeja amewataja wachezaji walioachwa kuwa ni Haruna Chanongo,Abuu Ubwa,Nasoro Masoud Chollo,Hassan Seif Banda na Philip Methusela.
Kwa upande wa wachezaji waliomaliza mkataba wao ,amesema ni Salum Kamana, na Elias Magul ambao amedai kuanzia sasa wako huru kujiunga na klabu yoyote na kuongeza kuwa wachezaji wengine wa timu hiyo wataendelea kuichezea Stand United msimu ujao.
Dkt. Maeja amesema kikao cha kamati ya utendaji kimeridhia kuwa Kenedy Nyangi kuwa katibu mkuu wa muda wa Stand United na Emmanuel Kaombwe kuwa katibu msaidizi mpaka pale atakapopatikana katibu kulingana na katiba ya klabu hiyo.
Mwenyekiti huyo wa Stand United amesema kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo mwenyekiti ana mamlaka ya kuteua wajumbe wawili wa kamati ya utendaji na kwamba tayari ameteua mmoja ambaye ni Sudy Rashid na nafasi nyingine iliyobaki ataitangaza siku nyingine.
Katika hatua nyingine Dkt. Maeja amesema kikao hicho cha kamati ya utendaji kimeunda kamati ya ufundi na usajili na kumtangaza bwana Geofrey Tibakyenda kuwa mwenyekiti wa wa kamati hiyo.
Mwenyekiti wa Acacia Stand United , Dr. Maeja amesema tayari uongozi wa Stand United umeanza kazi na orodha ya wachezaji wa timu hiyo na makocha wapya kutoka nje ya nchi watatangazwa siku chache zijazo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Geofrey Tibakyenda amewataja wajumbe wa kamati ya ufundi na usajili kuwa ni Richard Abwao,Meja Mohammed Ndalo,Mbasha Matitu,Mwalimu Gasper Coach na Sudy Rashid.
Tibakyenda amesema kamati yake itakamilisha usajili wake wiki chache zijazo na kocha msaidizi kutoka nchini Ufaransa Denis Guillume atakuwepo wakati wa usajili huo akishirikiana na kocha mkuu Patrick Leweg.
Viongozi hao wamewataka wananchi na wadau wa michezo mkoani Shinyanga kujitokeza kushirikiana na uongozi huo mpya ili timu hiyo iweze kushinda katika michezo ijayo.
Viongozi wapya wa Stand United waliochaguliwa Siku ya Jumapili wiki iliyopita ni Dkt. Ellyson Maeja aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa timu hiyo huku Richard Luhende akichaguliwa kuwa makamu mwenyekiti.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa ni Francisco Magoti, Geofrey Tibakyenda ,Jackline Burahi,Twahil Njoki na Mariam Richard.
Mwenyekiti wa Stand United Dkt. Ellyson Maeja akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya waandishi wa habari mjini Shinyanga
Dr. Maeja akisisitiza jambo
Mwenyekiti wa kamati ya Ufundi na Usajili katika Timu ya Stand United bwana Geofrey Tibakyenda akizungumza katika kikao hicho
Mwenyekiti wa kamati ya Ufundi na Usajili katika Timu ya Stand United bwana Geofrey Tibakyenda akisisitiza jambo
Kulia ni makamu mwenyekiti wa Stand United Bwana Richard Luhende
Mjumbe wa kamati ya Ufundi na Usajili,bwana Mbasha Matitu akitafakari jambo
Waandishi wa habari wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea
Kulia ni katibu msaidizi wa Stand United Emmanuel Kaombwe
Waandishi wa hbari wakitafakari jambo,kulia ni bwana Mbasha Matitu,mmoja wa wajumbe wa kamati ya Ufundi na Usajili katika timu ya Stand United
Tunachukua matukio...
Dr. Maeja akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari,Sam Bahari (wa kwanza kulia)
Makamu mwenyekiti wa Stand United,Richard Luhende akizungumza na waandishi wa habari,ambapo amewaomba wadau wa michezo ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga kuunga mkono uongozi mpya wa timu hiyo ili kuifanya timu ifanye vizuri katika michezo mbalimbali ijayo.
Kushoto ni Mwenyekiti wa Timu ya Stand United Dr.Ellyson Maeja akiteta jambo na mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Bwana Kadama Malunde ambaye pia ni Mkurugenzi wa Malunde1 blog
Mwenyekiti wa Timu ya Stand United Dr.Ellyson Maeja akiagana na mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Bwana Kadama Malunde baada ya kikao.
Picha zote na Frank Mshana na Kadama Malunde-Malunde1 blog