Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia ( FFU ) wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wamewasambaratisha viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ), waliokuwa wamehudhuria katika mkutano wa uzinduzi wa ‘Operesheni okoa Demokrasia’, katika uwanja wa CDT mjini humo kwa mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.
Askari hao walianza kufyatua mabomu ya kutoa machozi na kumwaga maji ya kuwasha kuanzia majira ya 9 alasiri, huku baadhi ya wananchi nao wakijihami kwa kurusha mawe, ambapo vurugu hizo zilidumu kwa zaidi ya saa moja na kusababisha maduka kufungwa, huduma za usafiri kusimama na baadhi ya wakazi wa maeneo yaliyopo jirani na uwanja huo wa CDT kujifungia ndani kutokana na moshi wa mabomu huku jamaa za wagonjwa waliolazwa katika zahanati ya Kahama Community wakilalamikia hali hiyo.
Zaidi ya watu 20 wakazi wa mji wa Kahama, akiwemo mratibu wa CHADEMA kanda ya Serengeti Renatus Nzemo wanashikiliwa na jeshi la polisi katika vurugu hizo za kuzima mkutano wa CHADEMA, ambao ulikuwa umehudhuriwa na wabunge saba wa chama, viongozi waandamizi wa chadema ngazi ya Taifa na kanda wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Mh. Freeman Mbowe.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa jioni la leo na Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya amepiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara hadi hali ya usalama itakapotengemaa.
Amesema Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu yoyote au chama chochote kitakachokaidi agizo hilo.
Social Plugin