Walimu Watano Waishi Darasani Kwa Miaka Mitatu Huko Simiyu




FAMILIA tano za walimu wa shule ya sekondari Shishani Kata ya Migato Halmashauri ya Itilima Mkoani Simiyu, zinaishi jengo la utawala tangu mwaka 2013.


Hali hiyo inatokana na ukosefu wa nyumba za walimu ambapo sasa shughuli za utawala shuleni hapo zinafanyika chini ya mti.


Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Tito Kwilasa alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, waliofika shuleni hapo kwa ajili ya kikao cha maendeleo ya kata kilichojadili changamoto mbalimbali zilizopo.


Kwilasa alibainisha kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 160, iliyoanzishwa mwaka 2007 ina uhaba mkubwa wa nyumba za walimu.


Nyumba za walimu zilizopo shuleni hapo ni mbili wakati kuna walimu 15 walioajiriwa, ambapo wanawake ni watatu na wanaume 12. Kwa sasa walimu hao wanaishi jengo la utawala, ambapo shule ina madarasa manne na maabara iliyofikia usawa wa madirisha.


‘’Kipindi cha mvua za masika inabidi kutoa darasa moja likachanganywe na lingine ili walimu tukakae darasani na kufanya shughuli za utawala huku wanafunzi hao wakikosa masomo,” alisema.


Alisema kuwa kipindi cha nyuma walimu walikuwa wachache, hivyo walibanana katika nyumba hizo mbili. Mwaka 2013 walimu waliongezeka, hivyo waligeuza jengo la utawala kuwa nyumba ya kuishi. Mwalimu mmoja alisema ni kero kubwa kwa familia hizo kuishi jengo la utawala ambalo pia halina vyoo.


Diwani wa Kata hiyo, Mbuga Ntobi alieleza kuwa watahakikisha walimu wanajengewa nyumba ili waishi katika mazingira ya ufundishaji.


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itilima, Kelisa Wambura alithibitisha kuwepo kwa hali hiyo. Alisema halmashauri imepanga kwenye bajeti ya 2016/17 kupunguza uhaba wa nyumba za walimu, hasa shule ya sekondari Shishani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post