SERIKALI imetangaza majina ya wanafunzi 24,258 waliokosa nafasi ya kujiunga na masomo ya kidato cha tano.
Akitangaza majina ya wanafunzi hao mjini hapa jana mbele ya waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisema idadi yao ambao ni sawa na asilimia 27.2 ya waliofaulu wakiwamo wasichana 6,789 na wavulana 17,739 wamekosa nafasi za kujiunga katika shule za sekondari za kidato cha tano na sita na vyuo vya ufundi vinavyomilikiwa na Serikali.
Alitaja sababu za wanafunzi hao waliofanya mitihani ya kumaliza elimu ya kidato cha nne mwishoni mwa mwaka jana kukosa nafasi hizo kuwa ni kutokana na ufinyu wa nafasi za shule na vyuo hivyo.
Pia aliitaja sababu nyingine kuwa ni kutimiza umri wa zaidi ya miaka 25 na kusababisha kutokuwa na sifa za kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano.
Lakini alisema wanafunzi hao waliokosa nafasi hizo ambao matokeo ya jumla ya mitihani yao ya kidato cha nne yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na kuonyesha kuwa walifaulu kwa asilimia 67.53, watadahiliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) katika fani za ualimu, afya, maendeleo ya jamii na kilimo.
“Tumeamua kutangaza majina hayo kutokana na ofisi yangu kuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu na kufuatilia shughuli za elimu katika mamlaka za Serikali kuanzia ngazi ya awali, msingi na sekondari. Pia Tamisemi itafanya uchaguzi wa awamu ya pili mara tu baada ya muda waliopewa wanafunzi kuripoti shuleni kupita,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliwapa angalizo wanafunzi waliopata nafasi ya kujiunga kidato cha tano katika shule za Serikali kuwa kama watachelewa kuripoti shuleni hadi ifikapo Julai 25, mwaka huu nafasi zao watapewa wanafunzi wengine.
Simbachawene alisema muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa kidato cha tano katika shule hizo utaanza Julai 11, mwaka huu.
Pia alitaja idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za Serikali na vyuo vya ufundi kuwa ni 64,961, huku wasichana wakiwa ni 28,911 na wavulana 36,050.
Akifafanua kuhusiana na kuchaguliwa kwa wanafunzi hao, alisema jumla ya shule 326 zikiwamo mpya 47 zimepangiwa wanafunzi wa kidato cha tano katika michepuo ya masomo mbalimbali.
“Jumla ya wanafunzi 64,961 wakiwamo wasichana 28,911 na wavulana 36,050 sawa na asilimia 71.98 ya wanafunzi 90,911 waliostahili kuingia kidato cha tano kwa mwaka huu wamechaguliwa.
“Idadi hiyo imeongezeka kwa wanafunzi 9,958 sawa na asilimia 18.1 ikilinganishwa na wanafunzi 55,003 waliochaguliwa mwaka jana,” alisema.
Simbachawene alisema kati ya wanafunzi 34,064 waliochaguliwa wakiwamo wasichana 13,466 na wavulana 20,590 sawa na asilimia 52.44 watajiunga na masomo ya sayansi na hisabati.
Pia alisema wanafunzi 30,897 wakiwamo wasichana 15,445 na wavulana 15,423 sawa na asilimia 47.56 wamechaguliwa kusoma masomo ya sanaa na biashara.
Alisema jumla ya wanafunzi 759 wakiwamo wasichana 220 na wavulana 539 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi.
Alisema idadi hiyo imeongezeka kwa wanafunzi 280 sawa na asilimia 58.48 ikilinganishwa na wanafunzi 479 waliochaguliwa mwaka jana.
Kuhusu sifa za kuwachagua wanafunzi hao, alisema kulingana na utaratibu uliowekwa na Serikali sifa zilikuwa ni yule aliyejaza fomu ya uchaguzi (selform).
Kwa kutumia fomu hiyo, alisema mwanafunzi anapaswa kujaza michepuo mitano ya masomo tofauti anayoyataka kusoma na shule anayotarajiwa kujiunga nayo kwa kila mchepuo.
“Ili kuwapata wanafunzi hao, Tamisemi hutumia mfumo wa kompyuta wa uchaguzi kumpanga mwanafunzi katika michepuo ya masomo yake na shule alizoomba kwa kuanzia na chaguo lake la kwanza.
“Kama mwanafunzi atakuwa hana sifa katika michepuo yote aliyoomba, mfumo wa kompyuta wa uchaguzi humpangia aliyefaulu zaidi na katika shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi kulingana na michepuo ya masomo na nafasi zilizopo katika shule husika,” alisema.
Pia aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha kila tarafa inakuwa na shule ya kidato cha tano ili wanafunzi wote wanaofaulu waweze kupata nafasi.
“Kutokana na ongezeko la ufaulu wa masomo ya sayansi, ninahimiza shule zitakazoanzishwa za kidato cha tano na sita ziwe na vyumba vitatu vya maabara za masomo hayo ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma sayansi,” alisema.
Via>>Mtanzania
Social Plugin