Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Wanafunzi Waliotimuliwa UDOM Wapinga Kuitwa VILAZA...Watishia Kuishitaki Serikali


Sakata Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) limezidi kupanuka baada ya wanafunzi waliorudishwa nyumbani kupinga kuitwa vilaza.



Jana wawakilishi wa wanafunzi hao ambao waliambatana na viongozi wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), walisema wanapinga pia hatua ya kutimuliwa chuoni.


Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Gibson Johnson alisema wanasikitika kuona wanavyozushiwa tuhuma mbalimbali kuhusiana na wao kujiunga na chuo hicho.


Alisema wamekuwa wakijiuliza sababu za Serikali zinazotaka kuhalalisha kutimuliwa kwao chuoni kuwa hawakuwa na sifa, jambo ambalo si la kweli.


“Siyo kweli kwamba sisi ni vilaza (wanafunzi wasiofanya vizuri darasani) na waliofeli na kupata daraja sifuri.


“Sisi ni wanafunzi tuliofaulu kwa viwango vilivyohitajika kwa daraja la kwanza hadi la tatu na tulipangiwa shule za kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita, lakini tulibadili na kuamua kujiunga Udom, hivyo tunaomba Serikali itumie busara zake.


“Hatuwezi kwenda kusoma kidato cha tano na sita kwa kuwa tumepoteza muda wetu.”


Alisema wanamshauri Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako na Rais John Magufuli kutumia busara kuwarudisha chuoni kumalizia masomo yao.


Katibu Mkuu wa TSNP, Alphonce Lusako aliitaka Serikali ichukukue hatua kwa waliohusika kudahili wanafunzi wasio na vigezo na kuwawajibisha.


“Lakini pia wanafunzi wafidiwe fedha na muda waliopoteza kwa wakati wote waliokuwa chuoni, kama hawatapewa haki zao, sisi tutashirikiana na wadau wa elimu zikiwamo asasi za utetezi wa kisheria kutafuta haki mahakamani,” alisema Lusako.


Udom yazungumza
Ofisa uhusiano wa Udom, Beatrice Baltazali alisema wanafunzi hao wote walifaulu vizuri wakiwa na daraja la kwanza, pili na wachache daraja la tatu.


“Wanafunzi wote walikuwa na nafasi ya kwenda kidato cha tano, lakini kwa kuwa waliahidiwa ajira, waliona wapitie huku kwa kuwa watapata ajira ya moja kwa moja,” alisema.


Beatrice alisema walimu wa Udom walikuwa wanalipwa fedha za ziada kuwafundisha wanafunzi wa programu hiyo kwa kuwa walikuwa wanatumia muda mwingi zaidi ya kiwango walichokuwa wamepangiwa.


“Kutokana na madai ya malipo hayo, mkaguzi wa ndani aligundua kuna tatizo, ndiyo walimu nao wakaamua kugoma, wanafunzi wakawa hawafundishwi Serikali ikaamua warudishwe nyumbani,” alisema Beatrice.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com