Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Waziri Mkuu: Kiongozi Yeyote Atakayedonoa Fedha Za Michango Ya Madawati Atakiona Cha Moto


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itamchukua hatua kiongozi yeyote atakayedonoa fedha za michango ya madawati inayotolewa na wadau mbalimbali wa maendeleo.


Pia amewaagiza watendaji wote wa Serikali, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, Maofisa Elimu, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, kuhakikisha michango hiyo inayotolewa inawafikia walengwa.


Aidha, amezitaka wilaya zote nchini zianzishe mpango endelevu wa kuhakikisha kwamba upungufu wa madawati unasahaulika kabisa katika maeneo yao na kwamba utendaji wa viongozi wa elimu na Serikali katika ngazi mbalimbali utapimwa kutokana na jinsi ambavyo wametekeleza maagizo hayo.


Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati wa matembezi ya hisani ya kukusanya fedha za kununulia madawati kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).


Katika maadhimisho hayo yaliyoanzia BOT hadi viwanjja vya Mnazi Mmoja, Gavana wa BOT, Profesa Benno Ndulu alimkabidhi Waziri Mkuu hundi ya shilingi milioni 263 zilizochangwa na benki hiyo pamoja na watumishi wake kama mchango wao kwa ajili ya ununuzi wa madawati.


Waziri Mkuu aliwapongeza watumishi wa BOT kwa kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto hiyo ambapo alitoa wito kwa taasisi zote katika sekta ya umma na binafsi pamoja na watu binafsi kuchangia uboreshaji wa elimu nchini kama sehemu ya “Majukumu ya Taasisi kwa Jamii” (Corporate Social Responsibility).


Amesema kuwa na elimu bora, siyo tu faida kwa Taifa, bali kwa waajiri pia, kwani itahakikisha kwamba taasisi za umma na binafsi zinapata wafanyakazi ambao wameiva na wenye weledi wa kutekeleza majukumu mbalimbali ya uzalishaji katika taasisi hizo.


“Nitoe wito pia kwa wanafunzi wote ambao watafaidika na kuboreshwa kwa mazingira ya kusomea, ikiwemo kupewa madawati na mahitaji mengine, kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwa faida yao na Taifa kwa ujumla na kwa kufanya hivyo, wanafunzi watakuwa wanaenzi jitihada za Serikali, taasisi za umma, taasisi binafsi na watu binafsi katika kuboresha elimu nchini,” amesema.


Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeazimia kupambana na changamoto za sekta ya elimu na kwamba tangu Uhuru, Serikali za Awamu zote zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali katika kuboresha elimu kwa wananchi wake.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com