Wananchi wakishuhudia ajali iliyohusisha mabasi mawili ya Kampuni ya City Boy, yaliyogongana uso kwa uso eneo la Kijiji cha Maweni, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana.
NI vilio kila kona. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya watu 29 kufariki dunia papo hapo katika ajali iliyohusisha mabasi mawili ya kampuni moja, yaliyogongana uso kwa uso eneo la Kijiji cha Maweni, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida jana.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, alisema ajali hiyo ilitokea saa 9:00 alasiri, baada ya mabasi mawili ya Kampuni ya City Boy kugongana uso kwa uso.
Alisema mabasi hayo, lenye namba za usajili T 531 DCE ambalo lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Kahama mkoani Shiyanga na jingine T 247 DCD lililokuwa likitoka Kahama kwenda Dar es Salaam yaligongana yalipokuwa yakipishana.
“Ni kweli ajali imetokea katika Kijiji cha Maweni kilichopo Manyoni, mabasi mawili ya kampuni moja ya City Boy yaligongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu 29.
“Kwa sasa tupo katika harakati ya kuwapeleka majeruhi hospitali na kuondoa miili ya watu waliopoteza maisha na kunasa kwenye vyuma vya mabasi hayo,” alisema Sedoyeka.
Alisema mabasi hayo yaligongana, kisha kuacha njia na kwenda porini, huku moja liliserereka na kuanguka chali.
Kamanda Sedoyeka alisema kati ya majeruhi, wengine wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana, na polisi wanaendelea kufanya uchunguzi.
“Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi kuhusu ajali hii ili tuweze kuelewa vizuri chanzo chake, hadi sasa taarifa ambazo tunazo ni pamoja na mabasi hayo yalikuwa kwenye mwendo kasi,” alisema.
Lakini taarifa zisizo rasmi zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zinaeleza kuwea madereva wa mabasio hayo walikuwa wakifanya mchezo waliouzoea wa kupishana kwa upande wa kulia kila wanapokutana tofauti na utaratibu wa kawaida wa kupishana kushoto.
Taarifa hizo zimedai kwamba dereva mmoja alipeleka gari lake upande wa kulia kama ilivyo kawaida yao, lakini tofauti na matarajio yake, mwenzake hakuhamisha gari lake hivyo kusababisha ajali hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Jackson Kitundu, alisema wamepokea majeruhi zaidi ya 20 na maiti mbili.
“Hadi sasa tumepokea majeruhi zaidi ya 20 na maiti mbili, bado majeruhi wengine wanaendelea kuletwa, ndiyo maana tunashindwa kutoa idadi kamili ya majeruhi waliopo, mpaka kesho (leo) tutajua tuna majeruhi wangapi,” alisema Dk. Kitundu.
Alisema majeruhi wengi waliofikishwa hospitalini hapo, hali zao zilikuwa zinaendele vizuri kidogo na wale wenye hali mbaya walikimbizwa mkoani Dodoma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwa, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai majeruhi wote wamepelekwa Hospitali ya Mkoa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Tuna msiba mkubwa, taifa limepoteza nguvu kazi, naomba mtuvumilie, kesho (leo) tutatoa taarifa kamili ya ajali hii,” alisema Mtigumwe.
MAJERUHI ASIMULIA
Mmoja wa majeruhi, Iddi Salum mkazi wa Kahama, akisimulia namna ajali hiyo ilivyotokea, alisema basi lililokuwa likitoka Dar es Salaam, lilihama njia na kuhamia upande wa pili wa basi lao ambalo lilikuwa linatoka Kahama, jambo ambalo lilisababisha yakutane uso kwa uso.
“Baada ya kuona hali hiyo, dereva wa basi letu lililokuwa likitoka Kahama ilibidi ampishe kwa kuhamia upande mwingine, lakini huyu mwingine akataka kurudi upande wake akashindwa, akajikuta anatugonga kwa nyuma na kupinduka matairi juu.
“Baada ya kugongwa nyuma, gari letu lilipoteza mwelekeo liliyumba, likaanguka na kuanza kuserereka juu ya barabara, huku watu wakipiga kelele kuomba msaada, siamini kama nimetoka na ninaongea muda huu… Mungu ni mwema,” alisema.
Naye Masha Alfa mkazi wa Dar es Salaam, ambaye ni fundi wa magari ambaye alikuwa kwenye basi la kutoka Kahama, alisema gari lao ndilo lilipoteza abiria wengi.
Alisema makosa yaliyofanywa na madereva wa mabasi yote kushindwa kuhimili mwendo kulichangia kutokea ajali hiyo.
“Natetemeka siamini kama nimepona, ila abiria wengi wamekufa,” alisema huku akilia kwa uchungu.
MIILI YAPOKEWA
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO), Marson Mwakyoma, alisema maiti 25 zilipokewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na majeruhi wanane.
MTANZANIA lilikuwepo eneo la tukio na kushuhudia miili hiyo ikishushwa kutoka kwenye lori aina ya Scania namba T 11O AJA pamoja na tela lake lenye namba T 241 AQQ.
Hospitalini hapo kulikuwa na askari wengi ambao miongoni mwao walikuwa wakishusha miili hiyo wakisaidiana na wauguzi na madaktari, huku idadi kubwa ya wananchi wakiwa wamezuiliwa nje ya geti la kuingilia.
RAIS MAGUFULI
Wakati huo huo, Rais Dk. John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopatwa na msiba huo kupitia RC Mtigumwa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli amepokea kwa masikitiko makubwa taaruifa za ajali hiyo.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hii ambayo imesababisha vifo vya watu 29, ambayo ni idadi kubwa ya Watanzania kwa hakika… nimesikitishwa sana, napenda kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki za marehemu hao katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” alisema Magufuli.
Alisema anamuomba mwenyezi Mungu awape uvumulivu, ustahimilivu wana familia wote waliopoteza ndugu na jamaa zao na kuwaombea marehemu wote wapumzike mahali pema peponi, amina.
Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wa ajali hiyo ambao wanapatiwa matibabu hospitali wapate nafuu, kisha wapone haraka ili waweze kurejea majumbani mwao na kuungana na familia zao katika shughuli za kila siku.
Hii ni ajali ya pili kutokea ndani ya siku nne, baada ya watu 11 kufariki dunia na wengine 47 kujeruhiwa mkoani Morogoro.
Ajali hiyo ya Morogoro, iliyohusisha magari matatu yaliyogongana, ilitokea eneo la Dumila, pembezoni mwa kibao cha Shule ya Sekondari Dakawa wilayani Kilosa barabara ya Morogoro kwenda Dodoma.
Watu watatu miongoni mwa waliofariki dunia waliteketea kwa moto uliosababishwa na ajali hiyo.
Via>>Mtanzania