Askofu
wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemjibu katibu mkuu wa
zamani wa CCM, Yusuf Makamba aliyemtuhumu kuwa ni mwongo akisema leseni
yake ni ya kuendesha magari makubwa na siyo vibajaji na maguta.
Akihubiri katika kanisa lake jana, Gwajima bila kutaja jina la Makamba, alisema: “Siwezi kushughulika na vigari vidogovidogo nyie mnanifahamu, mimi nina leseni ya kuendesha semi trailer …nadhani mmenielewa,” alisema huku waumini wake wakimshangilia.
Juzi,
Makamba aliwaeleza wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuwa Askofu
Gwajima ni kiongozi wa dini lakini ni muongo na kuwa uongo wake
unawaudhi hata waumini wake ambao ni wanachama wa chama hicho.
Alisema
Gwajima amekuwa akisema uongo kuwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete hataki
kuachia madaraka ya uenyekiti wa chama hicho, kitu ambacho Rais huyo
mstaafu alikanusha akisema ni yeye alikwenda kumshawishi Dk John
Magufuli kuchukua nafasi hiyo kabla ya muda wa uliopangwa kikatiba.
Katika
mahubiri hayo, Gwajima pia alisema mafunzo aliyoyapata tangu akiwa
mdogo ni kuogopa kugombana na watu wa aina tatu, walevi, wazee na
wagonjwa.
“Baba yangu alinifundisha nisigombane na walevi, wazee na wagonjwa kwani ukimpiga kidogo mtu wa aina hiyo anaweza kufa,” alisema Gwajima.
“Hata nyie waumini wangu nawaomba msigombane na watu wa aina hiyo kwani mnaweza kupata matatizo,” alisema.
Kiongozi
huyo aliongoza mamia ya waumini wake kumuombea Rais Magufuli kwa
kushinda uenyekiti wa CCM akisema kofia hizo mbili zimempa meno ya
kung’ata na zitamwongezea kasi ya kutatua matatizo ya wanyonge nchini.
Rais Magufuli juzi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya kupata kura zote 2,398 alizopigiwa na wajumbe wa mkutano huo.
Kutokana
na ushindi huo, Gwajima alisema Magufuli amepewa meno ya `kung’ata’
kila upande tofauti na alipokuwa na kofia moja ya urais.
Alisema
kwa muda mfupi aliokaa madarakani, elimu ya msingi na sekondari
zimeanza kutolewa bure kitendo ambacho maskini na wanyonge wa nchi hii
wameanza kuuona mwanga.
Alisema
ataendelea kumwombea Magufuli kwa sababu kazi anazozifanya
zinawanufaisha wanyonge na maskini ambao kwa muda mrefu walipuuzwa
katika nchi yao.
“Kuchaguliwa
kwake kuwa mwenyekiti ni zawadi kwetu Watanzania, tuendelee kumwombea
kila siku ili aendelee kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi,” alisema.
Alisema
nafasi hiyo mpya itamwezesha kupambana na rushwa tatizo ambalo
ameonyesha kuwa `atalivalia njuga’ hata ndani ya chama hicho.
Mbali
na Rais Magufuli, Gwajima aliwaombea pia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu,
mawaziri na Spika wa Bunge kwamba Mungu awalinde ili wamsaidie Rais
kutekeleza majukumu yake.
Kwa
mwezi mzima, Askofu Gwajima amekuwa akitafutwa na Polisi baada ya
kusambaa kwa sauti inayosikika kama yake ikitaka Rais mstaafu Kikwete
afikishwe mahakamani kwa makosa yote yaliyofanyika katika utawala wake.
Katika
mkanda huo, sauti hiyo inadai baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu
mikoani kupiga kampeni ya kutaka Magufuli asipewe uenyekiti ambao
umekuwa ukishikiliwa na Kikwete.
Baada
ya sauti hiyo, Gwajima aliondoka nchini kwenda Japan lakini Polisi
waliendelea kumsaka hadi Julai 12 walipomkamata katika Uwanja wa Mwalimu
Julius Nyerere (JNIA), aliporejea. Alihojiwa na kuachiwa siku hiyohiyo.