Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Bavicha -"Azma Yetu Kufanya Kikao Cha Kamati ya Utendaji Mjini Dodoma Ipo Palepale"

Ikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Mkutano Mkuu wa CCM kufanyika, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limesema azma yao ya kufanya kikao chao cha kamati ya utendaji mjini Dodoma ipo palepale. 

Julai 16, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema kikao cha Bavicha hakitofanyika kwa sababu itakuwa ni mwendelezo wa vurugu zao. 

Mkutano Mkuu wa CCM, utakuwa na ajenda mbalimbali ikiwamo ya Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete kumkabidhi kijiti cha uongozi Rais John Magufuli. 

Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita jana alisema  baraza hilo lipo kwenye hatua ya mwisho ya maandalizi ya kikao hicho kitakachohudhuriwa na zaidi ya wajumbe 50 kutoka mikoa yote. 
“Wajumbe wataanza kuwasili kesho (leo) mjini Dodoma. Hatuna wasiwasi na kikao hiki kwa sababu ni cha ndani siyo mkutano wa hadhara, ambao umepigwa marufuku na polisi,” alisema Mwita. 

Mwita alisema kikao hicho kitakuwa cha siku mbili kuanzia Julai 20 hadi 21 na kwamba, kitahudhuriwa na mameya na wenyeviti vijana wa halmshauri zinazoongozwa na Chadema. 

Alipotafutwa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob ambaye ni mwanachama wa Bavicha kujua kama atahudhuria kikao hicho alijibu: “Nitakwenda kwa sababu mimi ni kijana, sina sababu ya kukataa wito wa viongozi wangu wa juu wa Bavicha taifa.” 

Kuhusu kauli ya Kamanda Mambosasa, Mwita alisema polisi ilishatoa maelekezo ya kuruhusu vikao vya ndani. 

“Taarifa ya Mambosasa hatujaishangaa kwa sababu ni desturi yake kujichanganya, leo anasema hivi kesho vile. Tunamtaka atulie asubiri tumpe taarifa ni wapi kikao chetu kitanyika kwa njia ya amani,” alisema Mwita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com