MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Iringa imemtia hatiani askari Polisi, Pacificius Cleophace
Simoni, kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia ya mwanahabari Daudi
Mwangosi yaliyotokea Septemba 2 mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo
wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Kwa
mara ya kwanza Simoni alifikishwa mahakamani hapo Septemba 12 mwaka
2012 akituhumiwa kufanya kwa kukusudia mauaji hayo wakati mwandishi huyo
alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari kwenye
ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Ushahidi
uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri umeilazimisha
mahakama hiyo chini ya Jaji Kihwelo kuibadili kesi hiyo kutoka kwenye
mauaji ya kukusudia na kuwa mauaji ya bila kukusudia ambayo hukumu yake
ameisogeza mbele hadi kesho kutwa Jumatano.
Baada
ya mabadiliko hayo, wakili wa upande wa Jamhuri, Adolph Maganga,
aliiomba mahakama hiyo imhukumu mtuhumiwa huyo kifungo cha maisha jela
kwa mujibu wa Kifungu cha 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu huku wakili
wa utetezi, Lwezaula Kaijage akiiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu
kwa kumfunga kifungo cha nje.
Wakati
akitetea hoja yake ya kuiomba Mahakama itoe adhabu ndogo ya kifungo cha
nje kwa mtuhumiwa huyo, Lwezaula aliisihi mahakama hiyo imuonee huruma
mtuhumiwa huyo kwa kosa alilolifanya bila kukusudia kwa sababu ni kijana
mdogo mwenye miaka 27 anayetegemewa na Taifa kama nguvu kazi.
“Na
alishiriki operesheni iliyosababisha maafa hayo bila ridhaa yake,
amekaa mahabusu kwa miaka minne na katika kipindi hicho atakuwa amejutia
sana kosa lake, amefiwa na wazazi wake wote wawili, ana wadogo zake
watano wanaomtegemea na ana mke na mtoto mmoja mdogo,” alisema wakili huyo wakati akitoa ombi hilo.
Kwa
msingi huo, wakili huyo alitumia Kifungu cha 38(11) cha Sheria ya
Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kuomba Mahakama imhurumie mtuhumiwa huyo na
kumfunga kifungo cha nje.
Akisoma
maelezo ya kesi hiyo kabla ya kuibadili na kuwa na mauaji ya bila
kukusudia, Jaji Kiwehlo alisema upande wa Jamhuri ulileta mashahidi
wanne ambao kati yao watatu walitoa ushahidi ulioshindwa kuithibitishia
moja kwa moja Mahakama kama mtuhumiwa huyo alikusudia alipofanya mauaji
hayo.
Huku
akishangaa kwa nini Jamhuri pamoja na kuwa na rasilimali za kutosha
ilishindwa kuwaleta mashahidi wengine muhimu kama Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Iringa wa wakati huo, Michael Kamuhanda na Ofisa Upelelezi wa
Mkoa Wankyo, aliwataja mashahidi hao kuwa ni Said Mnuka, Azel Mwampamba
na Lewis Obado ambao pia wote walikuwa askari Polisi wa vyeo tofauti.
Alisema
ushahidi pekee uliomtia hatiani mtuhumiwa huyo ni ushahidi uliotolewa
na shahidi namba tatu ambaye ni mlinzi wa amani, Flora Mhelela.
Mlinzi
huyo wa amani aliwasilisha mahakamani hapo ungamo la mtuhumiwa huyo
lililomhusisha na mauaji hayo na ambalo wakati likiwasilishwa upande wa
utetezi haukulikana pamoja na kwamba ulikuja kulikana baada ya ungamo
hilo kuwasilishwa mahakamani hapo.
Kwa
kupitia ungamo hilo ambalo Mahakama imejiridhisha bila shaka yoyote
kwamba maelezo yake yalitolewa kwa hiari na mtuhumiwa huyo; mtuhumiwa
huyo alikiri kuhusika na mauaji hayo japokuwa alisema yalikuwa ni ya
bahati mbaya.
Sehemu ya ungamo hilo lililosomwa mahakamani hapo kwa mara nyingine tena na jaji huyo linasema;
“Niliondoka kutoa msaada nikiwa na long range ambayo ni silaha
inayotumika kupigia mabomu ya kishindo na machozi kama inavyoonesha
katika gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012.”
“Pale
katika eneo la tukio bila kujua wala kufikiria likafyatua bomu,
likafunguka likamuua mwandishi Daudi Mwangosi na kumjeruhi OCS ambaye
alikumbatiwa na marehemu, pia kuwajeruhi askari wengine watatu waliokuwa
karibu yangu na marehemu.”
Watu
mbalimbali walijitokeza kusikiliza kesi hiyo ni pamoja na Rais wa Klabu
za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo na Makamu
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deudatus Balile.
Wengine
waliojitokeza kuhudhuria kesi hiyo ni pamoja na wanaharakati wa haki za
binadamu, wanahabari wa Mkoa wa Iringa na wananchi wa Manispaa ya
Iringa.