Utafiti mpya umeonesha kwamba
wanaume wa Uholanzi ndiyo warefu zaidi duniani, na upande wa wanawake,
wanawake wa Latvia ndiyo warefu zaidi.
Kimo cha wastani kwa wanaume
Uholanzi ni futi 6 kwa sasa (sentimeta 183), na kimo cha wastani kwa
wanawake wa Latvia ni futi 5 inchi 7 (sentimeta 170).
Utafiti huo,
ambao matokeo yake yamechapishwa kwenye jarida la eLife, umefuatilia
kimo cha watu na mabadiliko yaliyotokea katika mataifa 187 tangu 1914.
Utafiti
huo umebaini kwamba wanaume wa Iran na wanawake wa Korea Kusini ndio
walioongeza kimo zaidi, wakiongeza kimo cha wastani kwa zaidi ya inchi 6
(sentimeta 16) na inchi 8 (sentimeta 20) mtawalia.
Wanawake wafupi zaidi duniani wanapatikana nchini Guatemala huku wanaume wafupi wakitokea Timor Mashariki.
Mwanamke wa umri wa miaka 18 kwa wastani nchini Guatemala alikuwa na
kimo cha futi 4 inchi 7 (sentimeta 140) mwaka 1914 utafiti wa kwanza
ulipofanywa na sasa kiwango hicho hakijafika kabisa futi 4 inchi 11
(sentimeta 150).
Kimo cha wastani kwa wanaume Timor Mashariki ni futi 5 inchi 3 (sentimeta 160).
Watafiti
hao wanasema kuwa chembe chembe za jeni hubadilikabadilika, lakini cha
muhimu zaidi ni kuwepo kwa lishe bora, usafi na matibabu ya hali ya juu.
Mataifa yenye wanaume warefu zaidi duniani 2014 (kwenye mabano ni nafasi iliyoshikiliwa 1914):
- Uholanzi (12)
- Ubelgiji (33)
- Estonia (4)
- Latvia (13)
- Denmark (9)
- Bosnia na Herzegovina (19)
- Croatia (22)
- Serbia (30)
- Iceland (6)
- Jamhuri ya Czech (24)
Mataifa yenye wanawake warefu zaidi duniani 2014 (kwenye mabano ni nafasi iliyoshikiliwa 1914):
- Latvia (28)
- Uholanzi (38)
- Estonia (16)
- Jamhuri ya Czech (69)
- Serbia (93)
- Slovakia (26)
- Denmark (11)
- Lithuania (41)
- Belarus (42)
- Ukraine (43)