Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Kamati Kuu ya CCM Mkoa wa Kigoma Yawavua Uongozi na Uanachama Makada wake 7 Kwa Usaliti


Kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma imewafukuza uanachama wanachama wake saba wakiwemo viongozi wa chama hicho kutokana na usaliti wa chama walioufanya kwa chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kigoma, Dr. Amani Kabour alisema, uamuzi huo umetolewa katika kikao cha Halmashauri kuu cha mkoa kilichofanyika Julai 20, 2016 kilicholenga kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.



Kabour alisema sababu zilizochangia wanachama hao kuvuliwa uanachama ni pamoja na kukisaliti chama kwa kukihama wakati wa uchaguzi mkuu, vitendo vya kuwapigia kampeni viongozi wa vyama vingine kwa lengo la kuifanya CCM isishike dola kutokana na unafiki wa wanachama hao.


''Tumefanya tathmini na kubaini kuwa baadhi ya wanachama ambao siyo waaminifu kipindi cha uchaguzi mkuu, walikuwa wakikisaliti chama, wengine walihama chama, na wengine kushiriki kufanya kampeni kwa wagombea wa vyama vya upinzani”, alisema Kabour.

Aliwataja wanachama hao waliovuliwa uanachama kuwa ni Josephine Ntauheza aliyekuwa Mwenyekiti UWT Wilaya ya Uvinza, Majaliwa Kayandamila (Katibu Mwenezi Wilaya ya Uvinza), Asha Kiembwe (Mwenyekiti UVCCM Wilaya ya Uvinza), Asha Ibrahimu (Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kigoma mjini), Twaha Bishingwa (mchumi kata ya Rubuga akahamia ACT Wazalendo) Shabani Ngoregwa alisaliti chama na kujiuzuru na mwingine ni Damas.

Naye katibu wa jumuiya ya wazazi mkoa wa Kigoma Stanley Mkandawile alisema  Ibara ya 7 kifungu cha 14 na 15 inasema kuwa mwanachama atakayekisaliti chama kwa kupigia kampeni mgombea wa chama kingine atafukuzwa chama na kufutiwa madaraka aliyokuwa nayo.

Mkandawile alisema hatua zote zimefuatwa ambapo vikao vilianzia ngazi ya kata, kamati za maadili wilaya na kamati zote husika hadi halmashauri kuu ya ya chama ambayo inatoa maamuzi baada ya kufuata sheria zote na kuwashirikisha wahusika wa usaliti huo.


Mmoja wa waliovuliwa uanachama ,Josephine Ntauheza alisema katika kata ya Kazuramimba aliyokuwa akipiga kampeni kwa Chama Cha Mapinduzi zilishinda kwa kishindo kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani na kushangazwa na tuhuma za kukisaliti chama.


Alisema amesikitishwa na uamuzi uliochukuliwa na viongozi hao na kudai kuwa CCM ni chama kilichomlea kisiasa hawezi kusaliti chama hicho na kuomba iundwe tume itakayowasaidia kusikiliza madai yao ili waweze kurudishwa kwenye chama kwa kuwa tuhuma hizo siyo za kweli.

Ntauheza alisema  maamuzi ya chama ni ya fitina kwa kuwa hajafanya kitendo chochote cha kukisaliti chama na kusema kuwa hajaridhishwa na maamuzi hayo ambayo hayajazingatia utaratibu kwa kuwa maamuzi yalipelekwa halmashauri kuu ya mkoa kabla ya kuwaitisha katika ngazi za chini na kusema kuwa atakata rufaa kudai haki yake kwa kuwa bado anakipenda chama chake.

Na Rhoda Ezekiel -Malunde1 blog Kigoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com