MWENYEKITI
wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete,
amekata mzizi wa fitna kwa kutangaza rasmi kuwa Mkutano Mkuu Maalumu wa
CCM, utakaofanyika mjini Dodoma kesho utafanya kazi moja tu ya kumchagua
Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Kikwete
alisema hayo alipofungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwenye ukumbi wa
White House, makao makuu ya CCM, mjini hapa jana. Kauli hiyo ya Kikwete
inamaliza minong’ono ya muda kuwa hapangekuwa na kupokezana kijiti
katika mkutano huo.
Pia
kauli hiyo imezima madai kwamba kungekuwa na mchujo katika uchaguzi wa
Mwenyekiti, ambapo majina hadi matano yangependekezwa na Kamati Kuu na
kupelekwa katika Halmashauri Kuu ambayo ingekata mawili na kupeleka
matatu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu, ili yapigiwe kura kumchagua
Mwenyekiti.
“Ajenda
yetu kubwa leo (jana) ni moja tu; nayo ni kupendekeza Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili nayo
Halmashauri Kuu ya Taifa ipendekeze kwa Mkutano Mkuu wa CCM ili
achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM,” alisema Kikwete kwenye ufunguzi
huo wa Kamati Kuu, akitumia dakika tano tu, kisha wajumbe wakaendelea na
ajenda.
Rais Magufuli alichaguliwa kuongoza Tanzania Oktoba mwaka jana.
Katika hotuba yake hiyo ya jana, Kikwete aliwajia juu ‘wafitini’ walioombea chama hicho kife katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Alisema “Wapo
watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa na salamu za rambirambi.
Walidhani wataibuka. Hawakuibuka na hawataibuka kamwe.”
Kikwete
aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kilikuwa kikao chake cha mwisho
cha Kamati Kuu, kauli iliyobainisha wazi kuwa anang’atuka kumwachia
kijiti Rais Magufuli kuongoza chama.
Alisema
amekuwa Mwenyekiti wa Chama kwa miaka 10, hivyo aliwashukuru wajumbe wa
Kamati Kuu kwa kumsaidia katika kipindi chote hicho huku akisisitiza; “Bila msaada wenu CCM isingekuwa imara kama ilivyo hivi leo.”
Wakati
wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli alikuwa
akifahamika kama Tingatinga na kwenye mikutano kadhaa, Rais mstaafu
Kikwete aliweza kumuita kwa jina hilo.
Wakati
huo huo Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete jana alikagua
ukumbi wa mikutano wa CCM na kuoneshwa sehemu mbalimbali ambapo alisema
ameridhika na maandalizi ya mkutano kwamba yanaenda vyema.
Maeneo
mengine aliyotembelea ni mabanda ya mama na baba lishe, sehemu za
kutolea huduma za Benki na mabanda ya maonesho ya wajasiriamali.
Katika
ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, makamu
Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula, waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na
Michezo Nape Nnauye, msemaji wa CCM Christopher Ole sendeka, naibu
katibu mkuu wa CCM Bara Rajab Luhwavi na wajumbe wa Kamati Kuu Pindi
Chana na Mohamed Seif Khatib. Wajumbe wa mkutano Mkuu maalum wa CCm
walianza kuwasili jana na wengine wengi wanatarajiwa leo.
Social Plugin