KATIBU
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ameandika barua ya kujiuzulu nafasi
hiyo kwa Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais John Magufuli, lakini Rais
amekataa barua yake hiyo.
Badala
yake, Rais Magufuli amemtaka Kinana na manaibu katibu wakuu wawili na
sekretarieti nzima ya chama hicho, kuendelea na kazi.
Hayo yalisemwa na Rais Magufuli wakati akitoa hotuba ya kushukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu Malumu wa CCM, mjini hapa.
“Nimepata
barua ya Kinana ya kujiuzulu nafasi yake pamoja na wakuu wa idara za
sekretarieti. Nimeamua Kinana na sekretarieti yote waendelee kuwepo.
“Kama kutakuwa na haja baadaye nitaitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na siyo leo,” alisema Magufuli, akiwatangazia wajumbe hao wa kikao cha Mkutano Mkuu, ambacho ni kikao cha juu cha chama.
Alisema
kwa kuwa mkutano huo ndiyo wenye uamuzi wa mwisho kuhusu masuala ya
chama, hivyo anawauliza wajumbe kama wamekubaliana na pendekezo lake
hilo la Sekretarieti ya chama iendelee.
“Nawauliza
wajumbe mnaafiki?” Ambapo wote kwa kauli moja walisema; “Ndiyo.”
Magufuli alisema kulikuwa na watu waliokuwa wamejipanga kuchukua nafasi
hizo za sekretarieti, lakini “sasa imekula kwao”. Hakutaja watu hao.
Akiongeza kuwa; “Nitaendelea
kuwa na Kinana na nina imani yeye na sekretarieti nzima watasimamia
vizuri mambo kadhaa niliyoagiza yasimamiwe haraka.”
Magufuli
alisema CCM ni chama cha aina yake duniani, kwa kuwa kila upande kuna
fursa ya ushauri kutoka kwa wazee wastaafu (huku akiwataja kwa majina),
jambo linalofanya kazi iliyo mbele yake kuwa nyepesi.
Rushwa
Akizungumzia
kuhusu utendaji wa chama na upitiaji wa muundo wa chama, Magufuli
alionya kuwa katika uongozi wake mwanachama atakayetumia fedha kuomba
uongozi, hatapita.
Alikumbusha
wakati wa kuomba udhamini ili ateuliwe kugombea urais kupitia CCM,
kwamba alifika Iringa akakuta Wilaya moja wanachama wote wamenunuliwa,
akalazimika kwenda vijiji vya mbali kupata wadhamini.
Magufuli
alisema rushwa aliyosema iko ndani ya chama hicho, imekuwa ikiwanyima
haki wanachama wengine kugombea na matokeo yake, vyeo vimekuwa
vikishikwa na watu wenye fedha na kuacha watu muhimu kwa sababu hawana
fedha.
Vyeo kufutwa
Aidha,
aliahidi kuongeza maslahi ya wafanyakazi wa chama hicho lakini akaonya
kuwa kuna baadhi ya vyeo ambavyo haoni kama vina tija katika siasa za
sasa, ambavyo anafikiria kuviondoa.
Alitoa
mfano wa makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), walezi wa Umoja
wa Wanawake Tanzania (UWT), washauri wa Jumuiya ya Wazazi na chipukizi,
ambao alisema wengi ni wa umri wa kuanzia miaka nane mpaka 15, ambao
wanapaswa kuwa shuleni.
Mwenyekiti
huyo pia alisisitiza umuhimu wa mwanachama mmoja cheo kimoja na kuonya
kuwa hapendi kuona mawaziri, ndio wajumbe wa NEC, ndio makamanda wa
vijana na kusema hali hiyo inawanyima cheo wanachama wengine.
Mali za chama
Kuhusu
mali za chama hicho, aliagiza sekretari hiyo nayo kuzifuatilia,
kuziorodhesha na kuhakiki mali ipi inaingiza mapato yapi na yanakwenda
wapi.
Kuhusu
ada za wanachama wanaozidi milioni 8.7, ambao Mwenyekiti mstaafu,
Jakaya Kikwete alisema kama kila mmoja angelipa ada ya Sh 1,200 kwa
mwaka, chama hicho kingepata zaidi ya Sh bilioni nane na kuondokana na
ukata wa kutegemea ruzuku, Magufuli aliagiza uhamasishaji wa kulipia ada
ufanywe na malipo yawe kwa njia ya kielektroniki.
Kinana
Akizungumza
baada ya kurejeshwa madarakani, Kinana alisema baada ya kuandika barua
hiyo ya kujiuzulu na hata kuzungumza na Magufuli, amejikuta akigonga
mwamba na hivyo anajipanga kuomba tena kupumzika.
Alisema
alipokuwa akifanya kazi, kuna wakati alidhani yuko mwenyewe lakini
Mwenyekiti Kikwete, alimpigia simu na kumwambia kuwa anamuunga mkono,
jambo lililomtia moyo.