Waziri
Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowasa amemtaka
Rais John Magufuli kuwa na utamaduni wa kufanya mazungumzo na wanasiasa
wenzake ili kufikia muafaka wa mambo mbali mbali ya kisiasa nchini.
Lowasa
ameyasema hayo leo wakati wa mahojiano na Tido Mhando kupitia kipindi
cha Funguka kinachorushwa na Televisheni ya Azam. Lowasa amesema kuwa
siasa ni mazungumzo na siyo kutoa tu amri kama anavyofanya Rais
Magufuli.
Kadhalika Lowassa amesema kila mtu ana wajibu wa kuheshimu amani ya nchi na hakuna mtu mwenye hati miliki ya nchi hii.
“Serikali
haipaswi kuwa na ghadhabu, inapaswa kuwa na tabia ya kuzungumza. Sisi
sote ni Watanzania kwa nini tunaogopa kuzungumza. Mazungumzo ndiyo njia
bora ya kufikia maridhiano. Pia Rais Magufuli aitazame Zanzibar,
tunasikia watu wanashughulikiwa kwa njia mbalimbali, wanakamatwa, hivyo
hawezi kuikwepa Zanzibar kwani hilo ni suala lake.” alisema Lowassa.
Amesema
CHADEMA ipo sahihi kutangaza operesheni ‘Ukuta’ hapo Septemba 1, mwaka
huu na kwamba bado kuna nafasi ya kufanya mazungumzo kabla ya tarehe
hiyo kufika ili kuepusha hali ya migogoro itakayojitokeza siku hiyo
itakapofika.
Akizungumzia
barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukemea operesheni hiyo, amesema
barua hiyo imejaa ghadhabu zaidi kuliko kuongelea mambo ya msingi ambayo
vyama vya upinzani vimekuwa vikionewa.
Akiongelea
suala la wabunge wa upinzani kutoka na kususia bunge, Lowassa amesema
hali hiyo ilisababishwa na kutokuwepo kwa Spika Job Ndugai ambaye kwa
muda mrefu alikuwa nje ya nchi akiendelea na matibabu.
“Ndugai
angekuwepo haya yote yasingetokea kwakuwa ni mtu makini sana na hata
kwa Naibu Spika kuna tatizo la Kisaikolojia kwasababu aliingia bungeni
kwa njia zisizoeleweka na hivyo kumfanya kushindwa kuhimili kiti
vizuri,” amesema.
Hata
hivyo amempongeza Rais Magufuli na kudai kuwa amefanya vizuri katika
baadhi ya maeneo lakini kuna maeneo mengine ambayo angepaswa kuyapa
kipaumbele zaidi akitolea mfano wa elimu na kudai kuwa badala ya kuanza
na suala la madawati angeanza na kushughulikia maslahi ya walimu kwanza,
na kutoa kipaumbele kwa tatizo la ajira nchini hasa kwa vijana.
Kuhusiana
na harakati za Serikali kuhamia Dodoma, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu
CHADEMA amesema viongozi wote waliotangulia tangu enzi za Mwalimu
Nyerere walikuwa na ndoto za kuhamia Dodoma lakini kuna mambo yaliyokuwa
yanaingilia mipango hiyo na mwisho kushindikana.
“Napongeza
harakati na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia Serikali
yote Dodoma lakini napenda kuwaambia wasiende kwa kasi sana wasije
wakavunjika miguu,” ameongeza.
Kuhusiana
na hali ya kisiasa Zanzibar, Lowassa ametoa rai kwa Rais Magufuli
aangalie hali ya Zanzibar kwani yanayoripotiwa kuendelea visiwani humo
yanatia kichefuchefu ikiwemo watu kukamatwa na kuteswa.
“Tusiitenge
Zanzibar na badala yake juhudi za makusudi zifanyike kuweka mambo sawa
kwa kufanya mazungumzo kwani siasa ni mazungumzo,” amesisitiza Lowassa ambaye amedai kuwa ana matumaini makubwa ya kuingia Ikulu mwaka 2020.
Kuhusu
kashfa ya Richmond kumfanya aondoke CCM kwa hasira baada ya kukosa
ridhaa ya chama hicho katika kugombea Urais, Lowassa amesema hakuondoka
CCM kwa hasira isipokuwa alituhumiwa na kuhukumiwa bila kupewa nafasi ya
kusikilizwa.
“CHADEMA
sikujipeleka mwenyewe bali Kamati Kuu CHADEMA ilinifata na kuniomba
nijiunge nao katika kupeperusha bendera yao na mimi niliona ni
‘opportunity’ nzuri hivyo nikakubali nikajiunga nao na tukafanikiwa
kupata kura zaidi ya milioni sita, idadi ambayo siyo ndogo hata kidogo,”
amejinasibu Lowassa.