Majambazi Yaua Walinzi Wawili na Kupora Shilingi Milioni 65 Huko Moshi


Wakati jeshi la polisi likisema linajiimarisha, vitendo vya ujambazi vinazidi kuitikisa nchi baada ya kundi la watu wasiojulikana kuvamia ofisi za Kampuni ya Ahsante Tours ya mjini Moshi, kuua walinzi wawili na kuiba Sh 65.5milioni.


Tukio hilo limekuja siku chache baada ya watu wasiojulikana kuvunja duka la kubadilisha fedha la Chase Forex Bureau De Change la mjini Moshi na kuiba zaidi ya Sh120 milioni.


Mbali na tukio hilo, Juni 12 mwaka huu, watu watano wakiwa na bunduki aina ya SMG, walivamia mji wa Magugu wilayani Babati mkoani Manyara na kupora Sh2.5 milioni.


Tofauti na tukio hilo la Magugu, hivi karibuni Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam waliwaua watu watatu eneo la Masaki katika majibizano ya risasi na Polisi.


Ukiachilia matukio hayo, taarifa kutoka mikoa mbalimbali nchini zinaonyesha uporaji wa fedha na mali kwa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda, unazidi kushika kasi maeneo mbalimbali.


Wengi wa wanaolengwa na wahalifu hao ni wateja wanaotoka kuchukua pesa benki au wanaokwenda kuchukua fedha jambo ambalo limezua hofu kuwa huenda baadhi ya wafanyakazi wa benki wanashirikiana na wahalifu.


Lakini, tishio kubwa zaidi la uhalifu linatokana na kuibuka kwa makundi ya kihalifu yanayokuwa yamejihami kwa silaha za kivita, yakiwamo mabomu ya kurushwa kwa mkono, yakichinja raia na kupora.


Hivi karibuni, Polisi Jijini Dar es Salaam waliwaua watuhumiwa hatari wawili waliokuwa wamejihami kwa bunduki na mabomu, wanaotuhumiwa kuchinja watu nane Jijini Tanga na watatu Jijini Mwanza

Hali hii ndio imemsukuma Rais John Pombe Magufuli, kuwaagiza polisi kuhakikisha ‘wanawanyang’anya’ majambazi silaha haraka kabla ya kuwadhuru polisi ama raia wasio na hatia.


Uporaji Ahsante Tours
Tukio la mauaji ya walinzi wawili ofisi za Ahsante Tours, lilitokea usiku wa kuamkia jana, baada ya watu hao kuwazidi nguvu walinzi na kuwafunga kamba kisha kuwapiga kwa kitu butu kichwani.


Kampuni hiyo inamilikiwa na mfanyabiashara Cathbert Swai na mkewe Stella Shangali, ambao pia wanamiliki hoteli ya kitalii ya Weruweru River Lodge iliyopo Mailisita, nje kidogo ya mji wa Moshi.


Taarifa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ambayo ni moja kati ya kampuni zinazoongoza kwa kupokea watalii wengi, zinadai huenda tukio hilo ni mpango wa ndani.


“Kuna maswali mengi tunajiuliza. Walijuaje kuna kiasi hicho kikubwa cha fedha kama taarifa hazikutoka miongoni mwetu?” alihoji mmoja wa wafanyakazi aliyeomba jina lake lisitajwe.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, alisema kati ya fedha zilizoibwa, kulikuwa na Dola za Marekani (Sh50 milioni) na Sh15 milioni za Tanzania.


Walinzi waliouawa wametajwa kuwa ni Omar Mohamed (48), mkazi wa Matindigani Pasua na Dominick Cheddy (41), mkazi wa Mailisita na wote ni wenyeji wa mkoa wa Tanga.


Kamanda Mutafungwa alisema tukio hilo liligunduliwa saa 1.00 asubuhi na wasamaria wema waliotoa taarifa polisi, na uchunguzi wa awali umebaini watu hao walikata uzio wa ofisi hizo.


“Baada ya kuingia ndani ya jengo hilo la ofisi walivunja ofisi ya meneja mkuu na baadaye ofisi ya mhasibu ndio wakaiba Dola 23,300 na pesa za Tanzania Sh15 milioni,”alisema Kamanda Mutafungwa.


“Tunashuku kuwa huenda hao majambazi waliamua kuwaua hao walinzi baada ya hao walinzi kuwatambua. Bahati mbaya hawakuwa na silaha yoyote hata panga hawakuwa nalo,”alisisitiza.

Kamanda Mutafungwa alisema Polisi inamshikilia mtu mmoja ambaye inaonekana alikuwepo wakati mauaji na uporaji huo ukifanyika lakini, majambazi hao hawakumdhuru sehemu yoyote.


Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa, aliwataka wafanyabiashara kupeleka pesa benki badala ya kuzihifadhi ndani au ofisini na kuwataka pia kuimarisha ulinzi ikiwamo kuweka CCCTV Camera.


Alitoa wito kwa wananchi wenye taarifa za waliohusika na tukio hilo, kulisaidia Jeshi la Polisi kama ilivyotokea wiki moja iliyopita ambapo taarifa zao zilisaidia kuwatia mbaroni wahalifu mbalimbali 30.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post